Kaimu wa Rais Nigeria apanga upya baraza la mawaziri
11 Februari 2010Matangazo
Waziri wa Sheria Michael Aondoakaa amehamishwa katika wizara inayoshughulikia masuala maalum na nafasi yake imekwenda kwa waziri wa ajira. Waziri Aondoakaa alie pia Mwanasheria Mkuu ni miongoni mwa kundi la mawaziri waliopinga mito ya kumkabidhi Jonathan Goodluck madaraka ili kuziba pengo lililoachwa na Rais Umaru YarÁdua anapokea matibabu nchini Saudi Arabia tangu mwezi wa Novemba mwaka jana. Goodluck Jonathan alishika rasmi madaraka yake mapya siku ya Jumatano baada ya hatua hiyo kuidhinishwa kwanza na bunge siku ya Jumanne na baraza la mawaziri siku moja baadae. Kaimu wa Rais Goodluck Jonathan amesema kuwa amechukua jukumu la kuiongoza Nigeria katika mazingira yasiyo ya kawaida na amevipongeza vyombo vya usalama nchini humo kwa utiifu wake na kwa kujitolea kwa dhati kutimiza wajibu wa kulinda usalama nchini Nigeria ikikabiliwa na mtihani mgumu. Vyama vya upinzani nchini humo vimeipinga hatua ya bunge kuridhia Jonathan kushika hatamu za uongozi na kusema kuwa hatua hiyo si halali na inakwenda kinyume na Katiba ya taifa. Goodluck Jonathan ataiongoza Nigeria hadi rais Umaru Yar´Adua atakapopata nafuu na kurejea nyumbani. Mwandishi:Martin,Prema/RTRE