Kallas: EU kuchukua "hatua muhimu" wiki hii kuhusu Ukraine
15 Desemba 2025
Hayo yamesemwa Jumatatu na mwanadiplomasia mkuu Umoja wa Ulaya Kaja Kallas aliyesisitiza kuwa hilo linaendelea kujadiliwa:
"Kwanza kuhusu suala la kuifadhili Ukraine tunayo wiki ya kulijadili hilo kwa kina. Mada hizi na maamuzi tunayopaswa kufanya ili kuiunga mkono Ukraine, nadhani ni muhimu sana."
Viongozi 27 wa Umoja wa Ulaya watakutana mjini Brussels siku ya Alhamisi kujaribu kufanikisha mpango huo wa kuifadhili Kyiv kwa miaka ijayo. Hata hivyo Ubelgiji inayohifadhi mali zaidi za Urusi zilizozuiwa, inapinga mpango wa kutumia fedha hizo zipatazo dola bilioni 106 kama mkopo wa kufidia uharibifu uliotokana na vita vya Urusi nchini Ukraine . Ubelgiji inataka hakikisho la mataifa yote ya Ulaya kushirikiana kulipa fedha hizo ikiwa itahitajika hapo baadaye.