1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamala akubali rasmi uteuzi wa kugombea urais

23 Agosti 2024

Mkutano mkuu wa chama cha Democratic umeingia siku yake ya nne na ya mwisho ambapo Makamu wa Rais wa Marekani, Kamala Harris, ametoa hotuba yake ya kukubali uteuzi wa kugombea kwenye uchaguzi wa rais.

Marekani Chicago | Mgombea urais Kamala Harris
Kamala Harris amekubali uteuzi wake na kusema atakuwa rais wa Wamarekani wotePicha: Kevin Lamarque/REUTERS

Kamala Harris ametoa hotuba kubwa kabisa maishani mwake wakati akikubali uteuzi wa kuwa mgombea urais wa chama cha Democratic. Makamu huyo wa rais wa Marekani mwenye umri wa miaka 59 aliangazia matumaini na hadithi ya maisha yake, akionesha utofauti na maono ya mpinzani wake wa chama cha Reupblican Donald Trump.

Mgombea urais huyo ameahidi kuwa rais wa Wamarekani wote, bila kumbagua yeyote mwenye maoni tofauti ya kisiasa. Harris amekichangamsha chama chake na kuyafuta kabisa matokeo yaliyomuonesha Trump akiwa kifua mbele katika uchunguzi wa maoni kwa kipindi cha mwezi mmoja tangu Rais Joe Biden alipojiondoa kinyang'anyironi, kutokana na hofu kuwa kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 81 asingeweza tena kugombea.

Soma pia: Walz akubali rasmi kuwa mgombea mwenza wa Kamala Harris

Tim Walz alikubali rasmi uteuzi wa kuwa mgombea mwenza wa Kamala katika uchaguzi wa Novemba 5Picha: Brendan McDermid/REUTERS

Wademocrat hata hivyo wanafahamu kuwa Harris anakabiliwa na mchuano mkali katika uchaguzi wa rais wa Novemba 5, ambao kama tu ilivyokuwa katika mwaka wa 2020 huenda ukaamuliwa na kura chache tu katika majimbo muhimu.

Kutoka kwa Barack na Michelle Obama hadi kwa Bill Clinton, vigogo wa chama wameonya wiki nzima kuwa Harris ana kibarua kikali cha kumbwaga Trump mwenye umri wa miaka 78.

Trump, ambaye aliamini kuwa anakaribia kurejea madarakani dhidi ya Biden, ametikiswa na mabadiliko ya ghafla ya chama cha Democratic ya kumgeukia mwanamke mwenye umri mdogo zaidi -- na mwanamke wa kwanza Mweusi katika historia kuwa mgombea mkuu wa chama hicho.

Na sasa Mrepublican huyo anazidi kutumia mbinu za matusi na ubaguzi wa rangi dhidi ya mpinzani wake huyo Mdemocrat.

Akizungumza karibu na kizuizi cha mpaka wa Mexico kilichojengwa wakati wa utawala wake katika jimbo lenye mchuano mkali la Arizona, Trump aliangazia Alhamisi juu ya uhamiaji, mada ambayo Warepublican wanaamini ndio udhaifu mkubwa kwa Harris.

Kamala Harris: Uhusiano na Afrika

02:34

This browser does not support the video element.

Akisimulia hadithi za watu aliosema waliuawa na wahamiaji waliovuka mpaka kinyume cha sheria, alisema: "Wakati Kamala akitoa hotuba yake kwenye mkutano mkuu usiku wa leo, hatawataja waathiriwa. Hata hatotaja majina yao."

Kupanda kwa kasi kwa Harris kisiasa, kutoka kuwa makamu wa rais wa kwanza mwanamke, mweusi mwenye asili ya Asia Kusini hadi kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Democratic pia ina maana kuwa bado hajulikani sana kwa wapiga kura wa Marekani.

Harris mbaye ni mtoto wa baba Mjamaica na mama wa Kihindi, anaitumia hotuba yake kulishughulikia hilo. Ameeleza jinsi alivyolelewa na mama mchapakazi na anafahamu changamoto zinazozikabili familia zilizokumbwa na mfumko wa bei.

Ametumia hotuba yake pia kwa kusimulia kazi yake alipokuwa mwendesha mashtaka, akiangazia mapambano yake kwa waathiriwa wa unyanyasaji wa kijinsia na uhalifu wa bunduki, huku akipambana na Trump ambaye ni mtu wa kwanza aliyepatikana na hatia ya uhalifu kuwahi kugombea urais wa Marekani.

Ujumbe wa Harris umejikita zaidi katika uhuru ambao anasema Warepublican wanaushambulia, haswa katika kupinga uavyaji mimba na haki za kupiga kura.

reuters, afp, ap, dpa

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW