1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Harris aapa kuendelea na mapambano licha ya kushindwa

7 Novemba 2024

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris amesema kuwa amempigia simu Donald Trump na kumpongeza kwa ushindi wake katika uchaguzi uliofanyika juzi nchini humo.

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris
Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris Picha: Kevin Lamarque/REUTERS

Makamu wa Rais wa Marekani Kamala Harris amesema kuwa amempigia simu Donald Trump na kumpongeza kwa ushindi wake katika uchaguzi uliofanyika juzi nchini humo.

Akitoa hotuba yake ya kukubali kushindwa katika Chuo Kikuu cha Howard hapo jana, Harris alisema atasaidia kuhakikisha kwamba Trump anakabidhiwa madaraka kwa njia inayostahili ila akaongeza kuwa hayuko tayari kukumbatia maono aliyonayo kwa nchi ya Marekani.

Soma: Trump arejea Ikulu ya White House kwa ushindi wa kushangaza

"Kanuni ya msingi ya demokrasia ya Marekani ni kwamba, ukishindwa uchaguzi, kubali matokeo. Kanuni hiyo ndiyo inayoitofautisha demokrasia na mfumo wa utawala wa kifalme au udikteta. Na yeyote anayetafuta imani ya umma, ni sharti aitii. Wakati huo huo, katika nchi yetu, hatumtii rais wala chama ila tunaitii katiba ya Marekani."

Ikulu ya White House vile vile imesema kwamba Rais Joe Biden atalihutubia taifa baada leo na kwamba amedhamiria kuwepo na makabidhiano ya amani ya madaraka kati ya sasa na Januari 20, ambapo Trump atakula kiapo cha kuwa rais wa Marekani.