Kamala Harris aungwa mkono kugombea urais Marekani
23 Julai 2024Hatua ya haraka ya kumuunga mkono Kamala Harris inaashiria juhudi za chama cha Democratic kuweka kando mivutano ya ndani iliyodumu wiki kadhaa kuhusu mustakhbali wa kisiasa wa rais Joe Biden, na kuungana pamoja kwa jukumu zito la kumshinda Donald Trump zikiwa zimesalia siku 106 kuelekea uchaguzi wa Novemba.
Maafisa mashuhuri waliochaguliwa ndani ya chama cha Democratic, viongozi wa chama na mashirika ya kisiasa kwa haraka walimuunga mkono Harris baada ya Biden kujiengua. Kampeni ya Harris imeweka rekodi mpya ya mchango mkubwa kuwahi kutolewa katika kipindi cha saa 24 kwa kampeni ya urais nchini Marekani.
Kamala Harris amesema kwa pamoja wanapambana kujenga nchi ambamo kila mtu ana bima nafuu ya afya, kila mfanyakazi analipwa kwa haki, na kila mzee anastaafu kwa heshima. Ameongeza kusema suala la kulijenga na kuliimarisha tabaka la kati, litakuwa lengo muhimu litakalochukua nafasi muhimu na kuangazia urais wake.
"Kwa hiyo kwa siku na wiki zilizo mbele yetu, mimi pamoja nanyi, tutafanya kila kitu kilicho katika uwezo na mamlaka yangu, kukiunganisha chama chetu cha Democratic, kuliunganisha taifa letu, na kuushinda uchaguzi huu," aliongeza kusema Harris.
Harris pia alisema katika simu 106 zijazo wana kazi kubwa ya kufanya, kubisha hodi katika milango ya nyumba za watu na kuwapigia simu kuwashasiwhi wapige kura.
Kamala Harris aungwa mkono kwa kauli moja
Baadhi ya wajumbe wa majimbo mbalimbali walikutana Jumatatu usiku kuthibitisha wanamuunga mkono Harris, wakiwemo kutoka jimbo la Texas, na jimbo anakotokea la Carlifornia.
Kufikia Jumatatu usiku Harris alikuwa amepata wajumbe zaidi ya 1,976 anaowahitaji kushinda uteuzi wa chama katika kura ya kwanza, kwa mujibu wa majumuisho ya shirika la habari la Associated Press, AP. Hakuna mgombea mwingine aliyetajwa na mjumbe aliyeulizwa na shirika hilo.
Mwenyekiti wa chama cha Democratic katika jimbo la California, Rusty Hicks, alisema asilimia kuanzia 75 hadi 80 ya wajumbe wa jimbo hilo wamesema siku ya Jumanne wanamuunga mkono Harris kwa kauli moja.
Katika taarifa yake kuhusu majumuisho ya kura za wajumbe yaliyofanywa na shirika la AP, Harris amemshukuru rais Biden na kila mtu ndani ya chama cha Democratic aliyeweka imani yake kwake, na anatazamia kwa matumaini kuwarai Wamarekani wampigie kura.
(ape)