1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamanda wa Iran asema nchi hiyo haitaki vita na Marekani

Sekione Kitojo
2 Januari 2020

Kamanda wa ngazi ya juu wa Iran amesema Iran haijielekezi katika vita lakini haihofii mzozo wowote, shirika la habari  la Tasmin limeripoti  baada ya Trump kusema Iran iko nyuma ya maandamano ya kuipinga Marekani Iraq. 

Hossein Salami, Vizechef der iranischen Revolutionsgarde
Picha: Tasnim

Rais wa  Marekani Donald Trump aliishutumu Iran  kwa  kuchochea maandamano  katika  ubalozi wa  Marekani  nchini  Iraq siku  ya Jumanne  na  kusema  Tehran  inawajibishwa. Iran imekana shutuma  hizo. "Hatuielekezi  nchi  hii  katika  vita, lakini  hatuogopi vita  vyovyote na  tunawaambia  Wamarekani  kwamba wazungumze vizuri  na  taifa  la  Iran.

Kamanda wa jeshi la mapinduzi ya Iran Hossein SalamiPicha: pana

Tuna  uwezo kuwavunja  mara  kadhaa  na  hatuna  hofu," kamanda wa   jeshi  la  mapinduzi ya  Iran brigadia jenerali Hossein Salami alinukuliwa  na  shirika  hilo  la  habari  la  Tasnim  akisema. Trump alisema  katika  ukurasa  wa  Twitter  siku  ya  Jumanne  kuwa  Iran "itawjibishwa  kikamilifu  kutokana  na  vifo, ama  uharibifu utakaotokea, katika majengo  yetu yoyote.  Watalipa  kwa  gharama kubwa ! Hii si tahadhari, hiki  ni  kitisho." Baadaye  alisema  hataki vita  ama  kutarajia  kuingia  vitani  na  Iran.

Kiongozi  mkuu  wa  nchi  hiyo Ayatollah Ali Khamenei  jana alishutumu mashambulizi ya  Marekani  dhidi  ya  wanamgambo washirika  wa  Iran  nchini  Iraq, akiilaumu  Marekani  kwa  matumizi ya  nguvu  katika  nchi  hiyo  jirani  ya  Iraq.

Iran ililalamika  jana  kwa  mjumbe  wa  Uswisi , ambaye anawakilisha  maslahi  ya  Marekani  mjini  Tehran, kuhusiana  na kile  ilichokiita, "matamshi  ya  kuchochea  vita" yanayotolewa  na maafisa  wa  Marekani.

Kiongozi mkuu wa Iran Ayatollah Ali KhameneiPicha: picture-alliance/abaca/SalamPix

Uwiano tete

Iraq imekuwa  ikipata  taabu  kujiweka  katika  uwiano  tete kati  ya  washirika wake  Iran  na  Marekani  wakati  hali  ya  wasi  wasi  ikiongezeka kufuatia  kujiondoa  kwa  Marekani  katika  makubaliano  ya  kinyuklia ya  mwaka  2015  na  Iran.Uhasama wa  kikanda  kwa  sehemu fulani  unaonekana katika majeshi ya  usalama ya  Iraq; Marekani imetoa  mafunzo kwa  jeshi  la  nchi  hiyo, wakati  Iran  imekuwa ikitoa  msaada  jeshi  la  Kundi  la  Hashed al-Shaabi.

Jeshi  hilo limeasisiwa  mwaka  2014, na  jeshi  la  hashed  rasmi  ni sehemu  ya  majeshi  ya  serikali ya  Iraq na  kiongozi  wake  mkuu Faleh al-Fayyadh , pia  anatumika  kama mshauri  wa  taifa  wa usalama.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike PompeoPicha: Getty Images/AFP/S. Loeb

Maafisa  wa  Marekani  na  Iraq wameliambia  shirika  la  habari  la AFP kwamba  wanashangaa  kuona  vikosi  vya  jeshi  la  Hashed kuwekwa  katika  wiki  za  hivi  karibuni  ndani  ya  eneo  la  kanda ya  kijani, Green Zone, eneo  linalolindwa  ambalo  lina  ofisi  za serikali  na  balozi za  nje, na  pia  ofisi  za  Umoja  wa  Mataifa.

Kuingiliwa  kwa   viunga  vya  ubalozi  wa  Marekani  mjini  Baghdad kumesababisha  waziri wa  mambo  ya  kigeni  wa  Marekani Mike pompeo  kuahirisha  ziara  yake  nchini  Ukraine pamoja  na  mataifa mengine  manne. Pompeo  alitarajiwa  kuwasili  nchini  Ukraine  leo Alhamis.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW