Kamanda wa zamani wa LRA hatiani uhalifu wa kivita Uganda
14 Agosti 2024Kamanda wa zamani wa kundi la waasi la Lord's Resistance Army, LRA, Thomas Kwoyelo, ametiwa hatiani kwa makosa kadhaa ya uhalifu dhidi ya ubinadamu, katika kesi ya kwanza kabisaa ya mwanachama wa ngazi ya juu wa LRA kushtakiwa nchini Uganda.
Uamuzi huo wa jopo la majaji wa mahakaka kuu ulitolewa mjini Gulu, kaskazini mwa Uganda, ambako kundi la LRA liliwahi kuendesha uasi wake. Kwoyelo alikabiliwa na mashtaka yanayohusisha mauaji, uporaji, kuwafanya watu watumwa, ubakaji na ukatili miongoni mwa mengine.
Alikutwa na hatia katika makosa 44 kati ya 78 ya uhalifu uliotendeka kati ya 1992 na 2005. Kiongozi wa juu kabisaa wa LRA, Joseph Kony, anaaminika kuwa mafichoni katika eneo kubwa lisilo na udhibiti la Jamhuri ya Afrika ya Kati. Marekani imetoa kitita cha dola milioni tano kwa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwake.