Kamandi ya UM yazishutumu Korea kwa kukiuka makubaliano
26 Mei 2020Timu ya kimataifa ya uchunguzi ya UNC imefikia kauli moja kwamba Korea Kaskazini na Korea Kusini zilikiuka makubaliano hayo ambayo yamekuwepo tangu vita vya Korea kati ya mwaka 1950-1953. Makubaliano hayo yalikuwa ya kusitisha mapigano tu wala si mkataba wa amani.
Kamandi ya UNC inayoongozwa na jenerali kutoka Marekani, inasimamia masuala katika eneo hilo lenye ulinzi mkali lakini lisilo na shughuli za kijeshi (DMZ), kati ya mataifa hayo mawili ya Korea, ambayo kimsingi bado yanazozana kivita.
Kwenye taarifa, UNC imesema vikosi vya Korea Kaskazini vilifanya kitendo cha ukiukaji, vilipofyatua risasi nne katika kituo chake cha ulinzi kilichoko kusini mwa eneo hilo la DMZ.
Korea Kusini pamoja na maafisa wa Marekani wamesema wanaamini ufyatuliaji huo wa risasi ulikuwa kama ajali. Lakini UNC imesema uchunguzi haujaweza kuthibitisha ikiwa kilikuwa kitendo cha makusudi au kwa bahati mbaya.
UNC imeongeza kuwa Korea Kaskazini ilikiri kupokea maswali ya kutaka majibu na ufafanuzi zaidi kutoka kwa wachunguzi, lakini haijatoa majibu rasmi.
Aidha Korea Kaskazini haijatoa tamko lolote la hadharani kuhusu kisa hicho.
Saa moja na nusu baadaye, Korea Kusini nayo iliyakiuka makubaliano hayo ilipofyatua risasi mara mbili kuelekea Korea Kaskazini. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti ya UNC.
Wizara ya Ulinzi ya Korea Kusini ilisema inasikita na ripoti ya UNC, na kwamba ilikosa uchunguzi muhimu kuhusu kitendo cha Korea Kaskazini.
Wizara hiyo imeongeza kuwa Korea Kusini ilifuata taratibu kamili katika kujibu ufyatuliaji risasi uliofanywa na Korea Kaskazini.
Chanzo: RTRE