Kamata kamata yaendelea Sudan baada ya mapinduzi
28 Oktoba 2021Vikosi vya usalama vya Sudan vimefanya kamatakamata ya waandamanaji jana usiku wakiwemo viongozi watatu mashuhuri wanaopigania demokrasia.
Hayo ni kwa mujibu wa jamaa zao na wanaharakati wengine wakati shinikizo la ndani na nje ya nchi likiongezeka dhidi ya jeshi la nchi hiyo kufuatia mapinduzi yake.
Soma pia:Umoja wa Afrika waifungia milango Sudan
Ukamataji huo umekuja wakati maandamano ya kupinga mapinduzi hayo ya Jumatatu yakiendelea katika mji mkuu Khartoum na kwingineko, na biashara nyingi kufungwa kufuatia wito wa kufanya migomo. Uongozi wa kijeshi umewasimamisha kazi mabalozi sita, akiwemo balozi wa nchi hiyo katika Umoja wa Ulaya.
Televisheni ya taifa na ya Al-Arabiya zimesema mabalozi wa Sudan nchini China, Marekani, Ufaransa, Qatar na Geneva wameachishwa kazi. Umoja wa Afrika umesitisha uwanachama wa Sudan hadi pale serikali ya mpito iliyokuwepo itakaporudishwa madarakani.
Soma pia: Waziri Mkuu wa Sudan arejeshwa nyumbani
AU inapanga kuutuma ujumbe Sudan kufanya mazungumzo na pande pinzani. Benki ya Dunia pia imesitisha fedha za operesheni zake nchini Sudan, ambayo uchumi wake umeathirika pakubwa kutokana na miaka mingi ya uongozi mbaya na vikwazo.