1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamatakamata Ethiopia yaibua hofu ya ukandamizaji wa zamani

18 Agosti 2020

Tume ya Haki za Binadamu nchini Ethiopia imesema vyombo vya dola nchini humo vimewakamata zaidi ya watu 9,000 baada ya makabiliano makali yaliyozuka mwezi uliopita.

Äthiopien Fernsehansprache Abiy Ahmed, Ministerpräsident
Picha: Ethiopian Broadcasting corporation

Taarifa hizo zimezidisha wasiwasi kuwa serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed iliyosifiwa kwa kuleta mageuzi inarejesha enzi ya kutumia mbinu katili na za mkono wa chuma za tawala zilizotangulia.

Waziri Mkuu wa Ethiopia aliyeingia madarakani mwaka 2018 kwa ahadi ya mageuzi ya kisiasa katika moja ya mataifa yenye rikodi dhaifu kwa ukandamizaji barani Afrika, hivi sasa anakabiliana na uasi ulojitwika nembo ya ukabila ambao sasa umegeuka kuwa vurugu.

Mabadiliko yanayosimamiwa na Abiy yamefufua mizozo ya enzi na enzi kuhusu umiliki wa ardhi, rasilimali na hata madaraka katika ngazi ya chini ya utawala na sasa anakabiliwa na changamoto ya kuwalinda raia huku akitetea misingi ya uhuru na haki za wengine iliyomuwezesha kushinda Tuzo ya Amani ya Nobel mwaka uliopita.

Picha: Addis Standerd

Soma zaidiChama tawala Ethiopia chamchagua kiongozi mpya 

Mwanasiasa huyo kijana ameahidi Ethiopia itafanya uchaguzi huru na wa haki ifikapo mwaka 2021 utakaokuwa na mafanikio muhimu katika taifa hilo la pili kwa idadi ya watu barani Afrika.

Hata hivyo, tume ya haki za binadamu nchini Ethiopia imesema watu 9,000 wamekamatwa tangu shambulizi la bunduki lililomuua mwanamuziki mashuhuri nchini humo kuzusha maandamano yaliyosababisha vifo vya watu 178 kwenye mji mkuu Addis Abbaba na maeneo jirani ya mkoa wa Oromiya.

Hizo ni vurugu mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa tangu waziri mkuu ABiy alipoingia madarakani. Serikali ilipotakiwa kutoa ufafanuzi wa taarifa hizo imeonesha kuwa kurejesha utulivu ndiyo kipaumbele cha hivi sasa.

Soma pia Watu 240 wauawa Ethiopia

Msemaji wa waziri mkuu, Billene Seyoum ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa moja ya wajibu wa msingi wa serikali ni kuhakikisha usalama na uthabiti wa utawala wa sheria na kwamba hatua ambazo serikali imekuwa ikichukua wiki chache zilizopita zinadhihirisha nia yake kuimarisha utii wa sheria na katiba.

Maambukizi ya corona gerezani

Miongoni mwa waliokamatwa ni mwanaharakati wa upinzani Dejene Tafa, ambaye polisi ilimchukua kutoka nyumbani kwake usiku wa manane wa Julai 8. Dejene ni mhadhiri wa chuo kikuu na katibu mkuu wa chama cha Oromo Federalist Congress.
 

Mkewe aitwaye Aselefech Mulatu, amesema mumewe amekamtwa bila kufunguliwa mashtaka na hivi sasa amepatwa na ugonjwa wa COVID-19 akiwa gerezani.

Soma piaHRW yaitaka Ethiopia kurejesha huduma ya intaneti Oromia 

Taarifa kuhusu Dejene kuambukizwa virusi vya corona zimethibitishwa na msemaji wa wizara ya afya za Ethiopia, lakini amesema mwanaharakati huyo hivi sasa amepona COVID-19. Dejene alishawahi kufungwa jela kwa miaka miwili kwa kushiriki maandamano yaliyomwangusha waziri mkuu aliyetangulia.

Msemaji wa serikali ya mkoa wa Oromiya Getachew Balcha, amesema watu 7,126 wamekamatwa katika mkoa huo pekee na kuongeza kuwa hana taarifa juu ya idadi ambayo tayari wamefunguliwa mashtaka.

Picha: picture alliance/AP Photo/NTB scanpix/H. M. Larsen

Ukamataji wa watu ulikuwa jambo la kawaida katika tawala zilizotangulia nchini Ethiopia ambazo zilitumia vyombo vya dola kukandamiza wakosoaji wake. Wakati maandamano ya kuipinga serikali yalipofanikisha waziri mkuu Abiy kuingia madarakani, kiongozi huyo aliratibu juhudi za kuwatoa mamia kwa maelfu ya wafungwa wa kisiasa.

Soma pia Maoni: Kifo cha mwanamuziki maarufu nchini Ethiopia

Lakini sasa wanaharakati kama Fisseha Tekle ambaye ni mchambuzi wa masuala ya Ethiopia katika shirika la kimataifa la haki za binadamu la Amnesty International anashuku kuwa serikali ya Abiy inataka kutumia mbinu zile zile za watangulizi wake za kuwakamata maelfu ya watu na kuwatia korokoroni.

Chanzo: Reuters

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW