1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kamati ya "Electoral College" kumchagua rasmi Biden

14 Desemba 2020

Wajumbe wa kamati maalumu ya uchaguzi nchini Marekani maarufu Electoral College wanakutana kote nchini humo Jumatatu hii kwa ajili ya kumchagua rasmi Joe Biden kuwa rais ajaye wa taifa hilo

USA North Caroline | Zertifikat des Electoral College
Picha: Jonathan Drake/REUTERS

Jumatatu ni siku iliyowekwa maalumu kisheria kwa ajili ya mkutano wa wajumbe hao wa Electoral College. Kiuhalisia, wajumbe hao wanakutana katika majimbo yote 50 nchini humo pamoja na wilaya ya shirikisho ambayo si sehemu ya jimbo lolote la Marekani, District of Columbia, kupiga kura zao. Matokeo yatatumwa Washington na kujumlishwa katika kikao cha pamoja cha bunge kitakachofanyika Januari 6 na kuongozwa na makamu wa rais Mike Pence.

Kura za wajumbe hao zimeibua mvuto wa aina yake kwa mwaka huu ikilinganishwa na wakati mwingine wowote na hasa kutokana na kitendo cha rais Donald Trump kukataa kata kata kukubali kushindwa kwenye uchaguzi na kuendelea kutoa madai yasiyo na msingi wala uthibitisho kwamba kaibiwa kura.

Rais mteule Joe Biden anatarajiwa kulihutubia taifa baada ya kura hiyo ya jopo la Electoral CollegePicha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Biden anajipanga kulihutubia taifa usiku wa leo, baada ya wajumbe hao kupiga kura, huku Trump akiendelea kung'ang'ania madai yake hayo ya kuibiwa na kusema alishinda uchaguzi huo na kuupuuza kabisa urais wa Biden hata kabla ya kuteuliwa. Trump aliwahi kusema "hapana nina hofu juu ya taifa langu kuwa na rais asiye halali, hicho ndicho ninachohofia", wakati alipozungumza na kituo chake pendwa cha televisheni cha nchini humo, Fox News, siku ya Jumamosi.

Mahakama zaendelea kupuuza kesi za Trump.

Kufuatia wiki za chama cha Republican kuwasilisha mkururo wa kesi mahakamani za kupinga matokeo ya uchaguzi ambazo hata hivyo zilitupiliwa mbali kirahisi tu na majaji, Trump na washirika wa chama chake cha Republican wiki iliyopita walijaribu kuishawishi mahakama ya juu kabisa kuziondoa kura 62 za Biden zilizopigwa na wajumbe hao katika majimbo manne, ambazo huenda zilisababisha mashaka kwenye matokeo. Hata hivyo, majaji walikataa ombi hilo siku ya Ijumaa.

Biden alishinda kura 306 za wajumbe wa jopo maalumu Electoral College dhidi ya Trump aliyepata kura 270. Kwenye majimbo 32 pamoja na District of Columbia, sheria zinataka wajumbe hao kumpigia kura mgombea aliyepata kura nyingi za umma, mpango uliothibitishwa kwa kauli moja na mahakama ya juu mnamo mwezi Julai.

Biden azidi kupongezwa kwa ushindi licha ya Trump kukataa kukubali kushindwa

01:06

This browser does not support the video element.

Wapiga kura karibu kila wakati humpigia kura mshindi wa jimbo kwa sababu kwa ujumla wanakilinda chama chao. Na hakuna sababu ya kutarajiwa kasoro zozote mwaka huu. Miongoni mwa wapiga kura mashuhuri kabisa ni mfuasi wa chama cha Democrat Stacey Abrams wa Georgia na Gavana wa chama cha Republican Kristi Noem wa South Dakota.

Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika kwa teknolojia ya kawaida kabisa, ya kura ya karatasi. Wajumbe hao mmoja mmoja watapiga kura kwa ajili ya rais na makamu wa rais.

Jopo maalumu la wapiga kura Marekani Electoral College lilitokana na makubaliano yaliyofikiwa wakati wa uundwaji wa katiba nchini humo kati ya wale waliopendelea kumchagua rais kwa kura ya umma na wale waliopinga kuuachia umma mamlaka ya kuchagua kiongozi wao. Na baada ya hatua hii, imebakia hatua moja ya mwisho, nayo ni uapisho.

Mashirika: APE.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW