Rais wa IOC Bach asema uwanja wa ushindani ni mkubwa
18 Septemba 2015Tathmini hiyo itafanywa katika kila mji miongoni mwa miji mitano inayogombea nafasi hiyo. Miji inayowania nafasi ya kuwa mweneji wa michezo ya olimpik ya msimu wa kiangazi au joto 2024 ni Budapest,Hamburg, Los Angels, Paris na Roma.
Miji hiyo ilitangazwa rasmi kuwemo katika kinyangayiro hicho Jumatano , katika kile Rais wa Kamati ya Olimpik ya kimataifa Thomas Bach alichokieleza kuwa uwanja wa ushindani mkubwa. Kamati hiyo ya Olimpik ilikumbwa na kampeni ya kuvunja moyo kwa michezo ya Olimpik majira ya baridi 2022, ambapo miji ya St Moriz/ Davos Uswisi, Much Ujerumani na Krakow Poland iliamua kujitoa katika mipango ya kugombea baada ya kura za maoni ya umma kupinga .
Hivi sasa ili kurejesha tena imani, IOC imepitisha mlolongo wa mageuzi chini ya kauli mbiu " Ajenda 2020" yenye lengo la kurahisisha ugombeaji na pia kuwa ni rahisi kigharama kuandaa michezo ya Olimpik. Bach aliliambia Shirika la habari la Reuters kwamba, " Ili kuhakikisha kunapatikana uungaji mkono wa kutosha kutoka kwa raia, IOC inafanya pia utafiti wake wa siri wa maoni katika kipindi hicho hicho sambamba na miji yote mitano, ili paweze kupatikana matokeo muwafaka na baadae kuyapima.´
Lakini litakuwa jukumu la mji husika kufanya juhudi ya kupata uungaji mkono wa wakaazi wake, ikizingatiwa kwamba kuna njia nyingi tafauti na mifumo tafauti ya kisheria kote duniani. Hadi sasa jiji la Hamburg kaskazini mwa Ujerumani ndilo pekee linalopanga kuitisha kura ya maoni itakayofanyika Novemba 29 mwaka huu pakitarajiwa uungaji mkono mkubwa wa kuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpik 2024. Hamburg ilizinduwa kampeni yake wiki iliopita . Balozi wa Olimpik wa kampeni ya kupigania hamburg kuwa mwenyeji wa michezo ya majira ya kiangazi 2024 ni Alexander Otto , ameelezea kuvutiwa kwake na uungaji mkono wa wakaazi wa mji huo, jambo ambalo amelitaja kuwa ni muhimu.
Kwa upande mwengine Bach amesema pamoja na kwamba wanayakaribisha maamuzi ya Miji wagombea, lakini ili kuhakikisha uwazi na kutokuwa na upendeleo IOC itaandaa pia tathmini yake yenyewe. Akaongeza kwamba kile kinachoitwa Ajenda 2020 kimetoa matokeo mazuri katika mchakato wa kumpata mwenyeji wa michezo ya 2024 na kwamba hayo ni mafanikio .IOC itachangia dola milioni 1.7 fedha taslimu pamoja na huduma za maandalizi kwa kamati inayohusika na michezo ya Olimpik 2024.
Wakati michezo ijayo itafanyika mwakani mjini Rio Brazil, ile za majira za baridi 2018 Pyeongchang Korea Kusini na ya majira ya joto 2020 Tokyo Japan. Mshindi wa kinyanganyiro hicho cha kuwa mwenyeji wa michezo ya Olimpik majira ya joto 2024 ataamuliwa katika kikao cha Kamati ya Olimpik ya Kimataifa mjini Lima Peru Septemba 2017.
Mwandishi :Mohammed Abdul-Rahman, afp,rtr,dpa
Mhariri:Yusuf Saumu