1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kambi ya rais Macron yatwaa ushindi uchaguzi wa bunge

13 Juni 2022

Muungano wa kisiasa wa mrengo wa kati wa Rais wa Ufaransa umepata ushindi mwembamba katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa bunge dhidi ya muungano wa mrengo wa kushoto unaoongozwa na Jean-Luc Melenchon.

Frankreich Parlamentswahl | Emmauel Macron
Picha: Johan Ben Azzouz/MAXPPP/dpa/picture alliance

Taasisi huru za kutabiri matokeo ya uchaguzi zimesema kuna uwezekano mdogo kwa muungano huo kupanua mwanya wa uongozi wake katika duru ya pili ya uchaguzi huo utakaofanyika wikendi ijayo. 

Kulingana na wizara ya mambo ya ndani ya Ufaransa, muungano wa kisiasa wa mrengo wa kati wa Rais Emmauel Macron wa Ensemble umepata ushindi wa asilimia 25.75 wa kura katika duru ya kwanza ya uchaguzi wa bunge dhidi ya ule wa NUPES unaoongozwa na mwanasiasa mkongwe Jean-Luc Melenchon ulioibuka wa pili kwa asilimia 25.66.

Soma pia:Chanzo cha mzozo wa Mali na mshirika wake Ufaransa 

Hata hivyo gazeti la Ufaransa la Le Monde limesema leo Jumatatu kuwa hesabu zake zinaonyesha kuwa muungano wa NUPES ulikuwa umeshinda duru ya kwanza ya uchaguzi huo wa bunge, huku baadhi ya wanasiasa wenye kuegemea mrengo wa kushoto wakidai kuwa, matokeo rasmi ya uchaguzi huo yalionyesha kuwa kura zao zilipunguzwa.

Manuel Bompard, mmoja wa washirika wa karibu wa Melenchon ambaye pia anawania kiti cha ubunge wa Marseille amekiambia kituo cha televisheni cha LCI kuwa, wizara ya mambo ya ndani inataka kuonyesha kwa makusudi kwamba wagombea wa Macron wanaongoza.

Wanasiasa wenye kuegemea mrengo wa kushoto wadai kura zao zilipunguzwa

Kiongozi wa muungano wa kisiasa wa mrengo wa kushoto wa NUPES Jean-Luc MelenchonPicha: CHRISTOPHE SIMON/AFP

Bompard ameendelea kueleza kuwa baadhi ya wagombea ambao walitangaza hadharani kuunga mkono muungano wa NUPES lakini hawakuwania kama sehemu ya muungano huo, walipaswa pia kujumuishwa kwenye hesabu rasmi.

Awali mwanasiasa huyo aliandika kwenye mtandao wa Twitter kuwa takriban kura 200,000 za muungano wa NUPES hazikujumuishwa kwenye matokeo rasmi ya mwisho lakini hakuwasilisha ushahidi wowote kuunga mkono hoja hiyo.

Hata hivyo waziri wa fedha Gabriel Attal amepuzilia mbali matamshi ya Bompard, akisema kuwa wanasiasa wa mrengo wa kushoto daima wana tabia ya kukosoa na kutilia mashaka matokeo yasiowaridisha.

Soma pia: Wafaransa wapiga kura katika duru ya pili ya urais

Ingawa matokeo katika duru ya kwanza yanachukuliwa kama kipimo cha muelekeo wa kisiasa- mfumo wa duru ya pili ya uchaguzi ulioundwa mahsusi kwa ajili ya kuleta utulivu- unatarajiwa kuupendelea zaidi mrengo wa Macron.

Msemaji wa serikali Olivia Gregoire amesema leo, "Nadhani unahitaji kuitizama mechi hadi mwisho wake kabla ya kutoa maamuzi yoyote. Kampeni bado haijakamilika."

Macron ampasha Trump!

01:12

This browser does not support the video element.

Muungano wa kisiasa wa Rais unaonyesha kila dalili za kushinda idadi kubwa ya viti bungeni katika duru ya pili ya uchaguzi lakini taasisi huru za kutabiri matokeo ya uchaguzi zinasema bwana Macron bado huenda akapoteza ushawishi wake bungeni.

Kulingana na utabiri wa taasisi ya utafiti ya Elabe, Muungano wa Ensemble umetabiriwa kushinda kati ya viti 260 hadi 300 vya bunge ikimaanisha moja kwa moja muungano huo utakuwa na wingi wa viti katika bunge la Ufaransa lenye wabunge 577.

Taasisi hiyo imetabiri kuwa muungano wa mrengo wa kushoto utajipatia kati ya viti 170 hadi 220, idadi hiyo ikiwa ongezeko kubwa tofauti na matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2017.

Taasisi ya Ipsos hata hivyo imetabiri kuwa muungano wa Ensemble utajikingia ushindi wa viti vya bunge kati ya 255 hadi 295.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW