1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JangaUlaya

Kambi ya wahamiaji Ugiriki yateketea kwa moto

9 Septemba 2020

Maelfu ya waomba hifadhi katika kisiwa cha Lesbos cha nchini Ugiriki wamekimbia kunusuru maisha yao kufuatia moto mkubwa kuwaka kwenye kambi ya wahamiaji ya Moria.

Griechenland Großbrand im Flüchtlingslager Moria
Picha: Reuters/E. Marcou

Zaidi ya watu 12,000, wakiwemo watoto kadhaa, walikimbia huku na huko kutoka kwenye makontena na mahema wakati moto huo ulipoteketeza sehemu kubwa ya kambi hiyo iliyoelemewa na idadi kubwa ya wahamiaji.

Moto huo ulianza masaa kadhaa baada ya wizara inayohusika na uhamiaji kusema kwamba watu 35 kwenye kambi hiyo walikuwa wameambukizwa virusi vya corona.

Kikosi cha wazima moto kimesema sehemu kubwa ya Moria imeteketezwa lakini hakukuwa na ripoti ya majeruhi wala vifo, ingawa baadhi ya watu walipatwa na matatizo ya kupumua baada ya kuvuta moshi.

Picha zilizorushwa na kituo kimoja cha televisheni zilionesha moshi mweusi ukiwa bado unafuka nje ya kambi hiyo, masaa kadhaa baada ya moto kuanza jana usiku. Msimamizi wa zimamoto, Yorgos Ntinos, ameliambia shirika la habari la AFP kwamba asilimia 99 ya kambi hiyo imeungua.

Kambi ya wakimbizi ya Moria ilivyokuwa ikionekana kabla ya kuteketea kwa moto.Picha: Imago Images/Zuma/N. Economou

Soma zaidi: Ugiriki kuwafukuza wahamiaji walioingia baada ya Machi mosi

Msemaji wa serikali, Stelios Petsas, alisema huenda kukatangazwa hali ya dharura kote kisiwani humo na ripoti kuhusu moto huo bado zinafanyiwa uchunguzi.

Polisi zaidi wa kupambana na ghasia wamepelekwa mara moja Lesbos na baadaye hii leo kutafanyika kikao cha baraza la mawaziri kuzungumzia dharura hiyo, serikali imesema.

Petsas ameonya kwamba mamlaka sasa zinakabiliwa na jaribio zito la kuwatafutia makaazi waomba hifadhi hao ambao hawana pa kuishi kufuatia moto huo, lakini pia kuwatafuta na kuwatenga wale walioambukizwa virusi vya corona.

Shirika la habari la Ugiriki, ANA limesema moto huo mkubwa ulianza baada ya mvutano wa wahamiaji waliotakiwa kutenganishwa kufuatia kugunduliwa hao walioambukizwa virusi vya corona.

Moria tayari ilikuwa imewekwa karantini hadi Septemba 15, na ni watu wa usalama tu waliokuwa wakiruhusiwa kuingia kambini humo baada ya kupimwa joto la mwili.

Vipigo kwa wakimbizi Lesbos

This browser does not support the audio element.

Soma zaidi: Ugiriki yaomba Euro Milioni 480 kwa ajili ya wakimbizi

Mamia ya waomba hifadhi wanasemekana walijaribu kukimbilia kwenye eneo la bandari ya mji wa Mytilene, lakini walizuiwa na magari ya polisi, wakati wengine wakijihifadhi kwenye eneo la milima karibu na kambi hiyo na wengine waliozuiwa waliishia kulala chini.

Kundi linalosaidia wakimbizi la Stand by Me Lesvos limeandika kupitia ukurasa wa Twitter kwamba lilipata taarifa kwamba wakaazi wa kisiwa hicho waliwazuia wakimbizi hao kuingia kwenye vijiji vya karibu. Lilisema kambi nzima inawaka moto. Kila kitu kimeungua. Watu wanakimbia na nyumba zao zimeharibiwa kabisa.

Chanzo: Mashirika