Kamil: Wahusika mauaji ya El Fasher wafikishwe ICC
3 Novemba 2025
Mji huo uliokuwa chini ya himaya ya jeshi sasa unadhibitiwa na wanamgambo wa RSF.
Wakati huohuo,kiongozi mkuu wa kanisa katoliki Papa Leo XIV amerejelea wito wake wa vita kusitishwa na kufunguliwa njia ya kusafirisha msaada wa kibinadamu.Hali inaripotiwa kuwa mbaya kwenye eneo hilo la kaskazini la Darfur. Thelma Mwadzaya anaarifu zaidi.
Kwenye hotuba yake ya kila Jumapili katika uwanja wa kanisa la mtafatifu Petro, Papa Leo wa 14 alisikitishwa na taarifa zinazotokea Sudan hususan mji wa El-Fasher, jimboni Darfur ambako mapigano yameongezeka.
"Ni kwa masikitiko makubwa ninavyofuatilia taarifa kutokea Sudan, hasa mji wa El-Fasher ulioko Darfur iliyozongwa na mapigano.Mauaji ya kiholela yanayowalenga wanawake na watoto. Mashambulizi dhidi ya raia wa kawaida na vikwazo vingi dhidi ya juhudi za kibinadamu vinasababisha mateso yasiyo kifani kwa watu ambao wamechoshwa na kipindi kirefu cha vita.Tunamuomba Mungu awapokee waliofariki, kuwasaidia wanaoteseka na kuzigusa nyoyo za waliohusika. Narejelea wito wa wahusika wote kusitisha vita na kufunguliwa kwa haraka, milango ya kusafirisha misaada ya kibinadamu.”amesema kiongozi huyo wa kiroho.
Itakumbukwa kuwa mwezi wa Septemba,kiongozi huyo wa kanisa katoliki aliitolea wito jamii ya kimataifa kuziongeza nguvu juhudi za kidiplomasia za kumaliza baa hilo la kibinadamu na misaada kuwafikia walengwa.
Mwito wa wahusika kupelekwa mahakama ya ICC watolewa
Kwa upande mwengine,waziri mkuu wa Sudan, Kamil Idris, ametoa wito wa wahusika wa maovu na ukatili uliotokea mjini El-Fasher kushtakiwa kwenye mahakama ya kimataifa. Kwenye mahojiano yaliyochapishwa katika gazeti la Switzerland la Blick, Waziri Mkuu huyo alipinga wazo la vikosi vya kigeni kupelekwa nchini mwake ambako vita vimechacha tangu Aprili mwaka 2023.
Gazeti hilo la Blick likimnukuu linaeleza kuwa,”jamii ya kimataifa haijafanya vya kutosha, tunahitaji vitendo sio maneno matupu. Kila kosa la uhalifu lazima lifikishwe mahakamani ikiwemo ya kimataifa,” amesisitiza.
Ifahamike kuwa baada ya miezi 18 ya uvamizi, mapigano na madhila dhidi ya raia,wapiganaji wa RSF waliudhibiti mji wa El-Fasher uliokuwa ngome ya mwisho ya jeshi la Sudan kwenye eneo la Darfur.
Tangu hilo kutokea,duru zinaeleza kuwa wakaazi wameuawa,wizi kutokea, visa vya ubakaji kuripotiwa na mateso mengine kufanyika jambo lililoisukuma jamii ya kimataifa.Kwa mtazamo wake, Waziri Mkuu wa Sudan anaishinikiza Umoja wa Mataifa kuwaweka wapiganaji wa RSF kenye orodha ya makundi ya kigaidi.
Vita vya Sudan vimewauawa maelfu, kuwaacha mamilioni bila makaazi na kusababisha janga kubwa zaidi la kibinadamu duniani.Takwimu za shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji, IOM, za jana Jumapili zinaiweka idadi ya waliokimbia maeneo ya Kordofan kaskazini kuwa 36,825. Eneo hilo liko umbali wa kilomita chache kutokea mashariki mwa Darfur ambako wapiganaji wa RSF waliliteka wiki iliyopita.