Kamishna wa tume ya uchaguzi Kenya ajiuzulu
18 Oktoba 2017Afisa wa ngazi ya juu katika tume inayosimamia uchaguzi nchini Kenya IEBC amejiuzulu siku nane kabla ya uchaguzi wa rais na kuikimbia nchi hiyo. Katika taarifa aliyotoa akiwa New York afisa huyo Dr. Roselyn Akombe amewalaumu wenzake katika tume hiyo kuwa na upendeleo wa kisiasa huku akiongeza kuwa uchaguzi unaotarajiwa wa Oktoba 26 hautakuwa wa kuaminika.
Kujiuzulu kwa Dr. Roselyn Akombe ambaye ni miongoni mwa makamishna saba wa tume ya uchaguzi IEBC nchini Kenya, ni pigo la hivi karibuni kwa mchakato wa uchaguzi wa rais, katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki ambayo imetumbukia katika mgogoro mbaya zaidi wa kisiasa katika kipindi cha muongo mmoja uliopita.
Kwenye taarifa yake aliyoitoa akiwa New York, Akombe amesema katika hali ya sasa ya tume ya IEBC, haiwezi kuandaa uchaguzi wa kuaminika Oktoba 26, na hivyo hataki kuwa miongoni mwa wanaoukejeli uadilifu unaohitajika kwenye uchaguzi" Akombe ameongeza kuwa amekuwa akivumilia kwa miezi kadhaa katika tume hiyo huku akijiuliza swali la wajibu wake hasa katika tume hiyo. "Ameandika kuwa tume ya IEBC ipo matatani.
Katika mahojiano na shirika la habari la BBC, Akombe amesema alihofia maisha yake na hivyo hawezi kurudi katika nchi yake hivi karibuni. Katika taarifa yake, ameelezea kuwa baadhi ya maafisa wa tume ya uchaguzi katika siku za hivi karibuni wameelezea hofu za usalama wao hasa katika maeneo ambayo yamekumbwa na maandamano yanayofanywa na wafuasi wa upinzani NASA dhidi ya IEBC. Amewalaumu wenzake kwa kutaka kufanya uchaguzi hata wakati maisha ya maafisa wake na wapiga kura yamo hatarini.
Kulingana na Dr. Akombe, uchaguzi hauwezi kuwa wa kuaminika wakati ambapo maafisa wanapata maelezo kuhusu mageuzi ya teknolojia na mitambo ya kuwasilisha matokeo ya uchaguzi katika dakika za mwisho, na wakati mafunzo ya maafisa wao yanaharakishwa kufuatia hofu za kushambuliwa na waandamanaji. Amesema tume ya uchaguzi na maafisa wake pia wanatishwa na wanasiasa.
Dr. Akombe amesema muda haujapita sana wa kuizuia Kenya kutumbukia kwenye mzozo. Wanaohitajika ni watu wachache waadilifu wanaoweza kusimama imara na kusema hatuwezi kuendelea na uchaguzi kwa namna ulivyopangwa kwa sasa.
Akombe ambaye alichukua likizo kutoka katika kazi yake kwenye Umoja wa Mataifa ili kuhudumu kama kamishna katika IEBC ameliambia shirika la habari la BBC kuwa amekimbilia New York Marekani baada ya kupokea vitisho kutoka kwa watu asiowajua.
Mahakama ya juu nchini Kenya iliubatilisha ushindi wa rais Uhuru Kenyatta alioupata baada ya uchaguzi wa Agosti nane, na kuamuru uchaguzi kufanywa upya ndani ya siku 60. Mahakama hiyo ilisema kulikuwa na dosari katika kufuata taratibu na sheria za uchaguzi.
Wiki iliyopita, kiongozi wa upinzani Raila Odinga aliyepinga ushindi wa Kenyatta, alitangaza kujiondoa kwenye kinyang'anyiro hadi mageuzi yafanywe katika tume ya uchaguzi, na akaitisha maandamano ili kuyashinikiza mageuzi hayo kufanywa. Hali hizo zimezidi kuzusha mkanganyiko zaidi kuhusu hatma ya uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika wiki ijayo.
Mwandishi: John Juma/AFPE/RTRE
Mhariri: Iddi Ssessanga