KAMPALA : Uganda yakanusha kuwepo mpakani mwa DRC
10 Septemba 2007Jeshi la Uganda limekanusha repoti leo hii kwamba vikosi vyake vimejikusanya kwenye mpaka na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo licha ya kufikiwa kwa makubaliano mwishoni mwa juma ya kupunguza hali ya mvutano kati ya nchi hizo mbili.
Radio Okapi inayodhaminiwa na Umoja wa Mataifa mashariki mwa Jamhuri ya Kidemkrasi ya Congo imekariri duru za kijeshi zikisema kwamba wanajeshi wa Uganda wamepiga kambi katika maeneo kadhaa kwenye mpaka huo ambapo mfanyakazi wa kampuni ya mafuta ya Uingereza aliuwawa mwezi uliopita kwenye mapambano ya risasi na wanajeshi wa Congo.
Msemaji wa jeshi la Uganda Meja Felix Kulayigye ameliaambia shirika la habari la Uingereza Reuters kwamba sio kweli kabisa kwamba wamewaweka wanajeshi wao kwenye maeneo hayo wakati nchi hizo mbili zikiwa kwenye mazungumzo.
Inaelezwa kwamba jeshi la Congo liko kwenye hali kubwa ya tahadhari.