KAMPALA-Waislamu waandamana Kampala kupinga marekebisho yatakayowapa haki zaidi wanawake katika ndoa.
30 Machi 2005Mamia ya watu wengi wakiwa Waislamu,wameandamana mjini Kampala,Uganda wakipinga muswada wa sheria uliopendekezwa,utakaowapa haki sawa wanawake nchini humo katika masuala ya ndoa,kutengana na pia talaka.
Kiasi cha waandamanaji 3,000 walikuwa wakipiga kelele huku wakiwa wamebeba mabango yanayolaani sheria hiyo inayojulikana Muswada wa Uhusiano wa Nyumba.Waandamanaji hao walikuwa wanadai muswada kama huo utadhoofisha imani ya Kiislamu na utawalazimisha Waislamu kukubaliana na tamaduni za Kikristo.
Hata hivyo vikundi vya kutetea haki za wanawake nchini Uganda vimeupongeza muswada huo na kusema utawapa sauti kubwa wanawake wanayoihitaji katika maamuzi ya kifamilia,yakiwemo iwapo waume zao waongeze wake wengine,haki ya kuwataliki waume zao na pia kuwa na haki ya kugawana mali walizochuma wakiwa ndani ya ndoa mara ndoa hiyo itakapovunjika.
Muswada huo ambao haujapangiwa tarehe ya kujadiliwa,una lengo la kufanya mageuzi na kuimarisha sheria zilizopo nchini Uganda kuhusu,ndoa,kutengana na talaka.