1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampala yageuka mji uliotelekezwa

Lubega Emmanuel26 Machi 2020

Shughuli katika mji wa Kampala zimedorora kufuatia agizo kwa magari ya usafiri wa abiria kusimamisha shughuli zao kwa muda wa siku 14 kufuatia mkurupuko wa ugonjwa wa COVID-19 unaouhangaisha ulimwengu wote.

Uganda Überwachungskamera in Kampala
Picha: Reuters/J. Akrena

Polisi wameshuhudiwa wakikabiliana na watu waliojaribu kukiuka agizo hilo hasa waendeshaji pikipiki maarufu kama bodaboda.

Aidha ni wale tu wanaouza bidhaa za chakula ndio watabaki wakiendesha shughuli zao sokoni. Hii ni kufuatia kugunduliwa kwa visa vingine 5 vya ugonjwa wa COVID-19 sehemu mbalimbali za nchi.

"Si mzaha tena… maisha yamezidi kuwa magumu kwa watu wanaotafuta riziki ya kila siku Uganda." Miongoni mwa hao ni waendeshaji pikipiki za abiria maarufu kama bodaboda, wachuuzi masokoni na wabebaji mbao hawatakuwa na mizigo ya kubeba.

Akitoa ilani ya kusimamisha kwa muda wa siku 14 kwa usafiri wa umma, rais Museveni amefafanua kuwa lengo ni kupunguza mikusanyiko ya watu na pia kupunguza kasi ya kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19.

Hadi sasa watu waliotangazwa kuugua ugonjwa huo ni 14 nchini Uganda akiwemo mtoto mchanga ambaye babake alifanya safari fupi mjini Kisumu Kenya hivi karibuni. Bwana huyo anasakwa akisemekana kuwa mjini Kampala.

Usafiri wa umma nchini Uganda umesimamishwa kwa muda wa siku 14 ili kupambana na kasi inayoongezeka ya kuenea kwa virusi vya corona.Picha: Getty Images/ I. Kasamani

Aidha mtu wa kwanza kugunduliwa kuwa na COVID-19 kaskazini mwa Uganda ni mfanyabiashara ambaye hajawahi kuondoka nchini.

Wananchi walaumu rushwa uwanja wa ndege kwa kuenea maambukizi

Kile ambacho watu wanaelezea kuwa chanzo cha ugonjwa huo kuenea ni mienendo ya ufisadi kwenye uwanja wa ndege na pia hatua ya watu mashuhuri kuwapokea jamaa zao waliotoka ng'ambo na kutofuata maagizo ya karantini.

Kulingana na agizo lililotolewa kuhusu usafiri, magari binafsi yataruhusiwa tu kuwa na watu watatu ikiwemo dereva huku yale yote ya serikali yataegeshwa kwenye makao makuu ya utawala wa wilaya yatumiwe na makundi ya wafanyakazi wa afya kuitikia kwa haraka visa vitakavyoripotiwa vya ugonjwa huo.

Ijapokuwa masoko yatabaki wazi, ni wale tu wanaouza bidhaa za chakula ndio watakaobaki wakiendesha shughuli zao.

Watu wamehangaika kufika mjini kutokana na ukosefu wa magari ya abiria. Baadhi waliosikia tangazo hilo Jumatano jioni, waliamua kulala katika nyumba za wageni mjini. Baisikeli itakuwa chombo muhimu kwa wale wanaotaka kuja mjini kuendesha shughuli zao.

Mwandishi: Lubega Emmanuel