1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaMarekani

Kampeni ya Biden ya kugombea Urais 2024 na changamoto zake

25 Aprili 2023

Rais wa Marekani Joe Biden anajiandaa hapo mwakani kuanzisha kampeni ya kutaka kuchaguliwa kwa muhula wa pili madarakani, kampeni ya mwaka 2024 itakuwa tofauti mno na ile ya mwaka 2020 kutokana na changamoto kadhaa.

Irland, Ballina, | US Präsident Joe Biden
Picha: Leon Neal/Getty Images

 Rais Joe Biden, kutoka chama cha Democratic ametangaza siku ya Jumanne, nia yake ya kugombea tena Urais wa Marekani. Mwaka 2020, Biden hakusikika sana wakati janga la COVID-19 likiwa limesambaa kote nchini humo na kusababisha maafa makubwa na kugusa sekta muhimu. Lakini pia alikuwa si mzungumzaji sana wakati wa kampeni za uchaguzi alipochuana na Rais wa wakati huo Donald Trump, kutoka chama cha Republican.

Trump alikuwa akizungumza kwenye mikutano ya hadhara, huku kwa kiasi kikubwa Biden akifanya kampeni zake katika nyumba yake huko

Wilmington, Delaware, ili kuepuka umati wa watu na kuzuia kuenea kwa Covid-19 lakini pia kupunguza hatari ya yeye kuambukizwa virusi hivyo.

Hali hiyo itabadilika wakati huu. Biden hatoweza kukwepa tena mikutano, iwe mikubwa au midogo. Kampeni za mwakani zitarejea katika mfumo uliyozoeleka ambapo mgombea hulazimika kukutana na wapiga kura watarajiwa kwenye migahawa, viwandani na ofisi za vyama vya wafanyakazi na kudiriki shughuli kadhaa ikiwemo kupeana mikono, kupiga picha na mashabiki wake, na kukutana na umati wa watu.

Soma pia:Biden atangaza kuwania tena urais wa Marekani 

Rais wa Marekani Joe BidenPicha: Patrick Semansky/AP Photo/picture alliance

Mkutano mkuu wa Chama cha Democrats huko Chicago utafanyika kwa njia ya uhudhuriaji badala ya mtandaoni. Na Biden, ambaye kwa sasa ana umri wa miaka 80 na ambaye ndiye rais mwenye umri mkubwa zaidi katika historia ya Marekani, atakuwa na kibarua kizito wakati akitafuta ridhaa ya wananchi kwa muhula wa pili wa miaka minne zaidi madarakani.

Mwaka 2020, Biden alimshinda Trump kwa ushindi mwembamba baada ya kutwaa majimbo ya Pennsylvania na Georgia, na kupata asilimia 51.3 ya kura huku Trump akiambulia asilimia 46.8.

Kikwazo cha umri

Warepublican watafuatilia kwa karibu dalili zozote za kupungua kwa ratiba ya kampeni ya Biden ili kunadi kwamba umri wake mkubwa ni kikwazo cha kurejea Ikulu kwa muhula wa pili. Mwanamikakati wa Republican Scott Reed amesema inashangaza mno kwamba Biden anafikiria angeweza kuhudumu muhula wa pili, mbali na kipindi kilichosalia cha muhula huu.

Rais wa zamani wa Marekani, Donald TrumpPicha: EVELYN HOCKSTEIN/REUTERS

Trump ambaye ndiye chaguo la kwanza la chama cha Republican, mwenyewe ana umri wa miaka 76. Jibu la Biden kwa wasiwasi huu juu ya umri wake amekuwa akisema kuwa rekodi yake ya mafanikio ya kisheria ndio ishara ya ufanisi wake.

Mpanga mikakati wa chama cha Democratic Karen Finney amesema kuwa na ratiba pana ya safari za kampeni sio kipimo cha uwezo wa mgombea kufanya kazi na kwamba kunaweza kutumiwa mbinu nyingine za kuwafikia raia wa Marekani, lakini akasisitiza kuwa waRepublican watajaribu kufanya kila jambo ili kuonesha kuwa umri wa Biden ni kikwazo.

Ubunifu katika kampeni

Timu ya wasaidizi wa kampeni ya Biden walianzisha ubunifu katika kampeni yake ya mwaka 2020 wakati ugonjwa wa COVID-19 ulipokuwa umeenea kote nchini humo.

Baadhi ya ubunifu huo ulionekana kuwa mafanikio, haswa harakati za uchangishaji pesa mitandaoni bila kuhitaji usafiri wa gharama kubwa.

Soma pia: Biden kuwania tena urais 2024

Lakini mabadiliko mengine yalizusha utata zaidi, ikiwa ni pamoja na marufuku ya miezi kadhaa ya kufanya kampeni ya nyumba hadi nyumba na kitendo cha Biden kuonekana mara kwa mara katika ngome nyumbani kwake, jambo lililokemewa pia na wapiga kura wa mrengo wa kulia.

Lakini masuala mengine yanaweza kukwamisha kampeni ya Biden, ikiwa ni pamoja na masuala ya kiuchumi.

Mwanamikakati wa chama cha Republican Ford O'Connell anasema Wamarekani wengi walimpigia kura Biden kwa matarajio ya kurejea katika hali ya kawaida baada ya utawala wa Trump lakini tangu amekuwa madarakani mambo si shwari, hasa linapokuja suala la uchumi na mfumuko wa bei.

Wasiwasi wa kushuka kwa uchumi

Biden akiwa Ikulu ya White House 13.03.2023 akihakikisha kuhusu uthibiti wa uchumi na mfumo wa benki wa MarekaniPicha: Saul Loeb/AFP

Biden aliingia rasmi madarakani mwezi Januari mwaka 2021 wakati chanjo ya COVID

ikiendelea kutolewa na hali ya uchumi ikiimarika hatua kwa hatua baada ya vikwazo vya muda mrefu.

Soma pia: Trump atangaza kuwania urais 2024

Kwa sasa Marekani inajivunia nafasi za kazi milioni 3.2, ambazo ni za ziada tangu kuanza kwa janga la Covid19. Lakini Wamarekani wana wasiwasi juu ya kushuka kwa uchumi, na Biden atakuwa na wakati mgumu kutokana na muelekeo wa uchumi mnamo mwaka 2024, ambapo kuna uwezekano wa ukosefu wa ajira kuongezeka,   ukuaji wa uchumi kusuasua, viwango vya riba kubaki juu huku mfumuko wa bei ukiendelea pia.

Trump, ambaye tayari ametangaza nia yake ya kugombea tena Urais, anaweza kwa mara nyingine kuwa mpinzani wa Biden na anatarajiwa kufuata mkakati ambao aliutumia mwaka 2016 na 2020 kwa kufanya mikutano ya hadhara ili kujizatiti miongoni mwa wafuasi wake.

Lakini Trump atalazimika kwanza kushinda kibarua kigumu cha uchaguzi wa kuidhinishwa ndani ya chama chake cha Republican, jambo ambalo Biden, kama rais aliye madarakani hana upinzani mkubwa ndani ya chama chake.