Kampeni ya chanjo ya Covid-19 kwa raia wa Turkana
23 Machi 2022Idadi kubwa ya wafugaji wa kuhamahama wanaoishi katika jimbo la Turkana, wameendelea kupokea chanjo dhidi ya virusi vya corona kutokana na mpango wa wizara ya afya ya hapa, kuwafuata wafugaji hao katika maeneo ya kuwapa maji mifugo yao na kuwachoma sindano.
Hatua hiyo kulingana na wizara hiyo, ndiyo njia ya kipekee ya kuhakikisha jamii pana ya hapa inapokea chanjo kwani wengi wa wakaazi, huandamana na mifugo yao malishoni na huenda wakakosa kufikiwa na chanjo hiyo endapo hawatafuatiliwa.
Waziri wa afya wa turkana Jane Ajele, amebainisha kwamba, idara yake imekuwa ikitumia aina ya dozi ambayo inachomwa mara moja badala ya ile inayochomwa mara mbili.
"Tulionelea ni vyema tutumie dozi ya johnson and johnson ambayo inatumika mara moja tu na ikapendwa na watu wengi na hili limesaidia sana.”
Wizara hiyo imeeleza kwamba,angalau asili mia kumi na saba nukta tano ya wakaazi wa hapa wamepokea chanjo dhidi ya covid 19 tangu kuzinduliwa kwa mpango wa kuwafuata wafugaji katika sehemu zao za malishoni.
Soma pia→Wafugaji Turkana wabadili mfumo wa maisha kutokana na ukame
''Tunawapa huduma muhimu ''
Katibu wa serikali ya kaunti ya Turkana Peter Eripete,ametaja hatua ya kuwafuata wafugaji katika maeneo yao ya malisho kama iliyochangia ongezeko la idadi ya watu waliopokea chanjo ya covid 19 katika jimbo hili.
Akiongea alipoipokea timu ya DW ofisini mwake mjini Lodwar,Bwana Eripete ameeleza kwamba,serikali ya kaunti imekuwa ikitumia maeneo yaliko mabwawa kama sehemu mwafaka ya kutoa huduma kwa jamii ya wafugaji.
"Ukitaka kuwapata wafugaji,ni sharti uwatafute sehemu waliko na kwa wakati.Huwezi kuwatafuta malishoni lakini unaweza kuwapata kwenye vituo vya maji na wakati mwingine,inabidi tunawapa huduma muhimu wakiwa hapo kwenye maji hususan kwenye maswala ya chanjo kwa Wanyama na binadamu”.
Soma pia→Mapigano ya kikabila yauwa zaidi ya 300 Kenya 2015
Mapema mwezi huu,wizara ya afya ya kitaifa iliondoa uvaaji barakoa katika maeneo ya umma kutokana na kupungua kwa visa vya corona nchini.
Hadi kufika leo,ni watu milioni kumi na saba na laki tatu waliopokea chanjo ya corona kati yao watu milioni saba wakiwa wamepokea dozi kamili ya chanjo na idadi sawia na hiyo ikiwa inasubiri dozi ya pili kukamilisha dozi zao.
Takwimu za serikali zinaeleza kwamba,angalau asili mia sitini na nane ya wakenya hawajachomwa chanjo yoyote.