1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za uchaguzi Kenya zaingia dakika za lala salama

5 Agosti 2022

Kampeni za uchaguzi nchini Kenya zimeingia kwenye dakika za lala salama, huku wagombea urais wakitafuta kuwavutia wapiga kura ambao bado hawajafanya maamuzi juu ya nani watampigia kura.

Kenia Wahlen 2022
Picha: Baz Ratner/REUTERS

Kulingana na sheria za Kenya, kesho Jumamosi tarehe 6, saa 12 jioni ndiyo siku ya mwisho ya kampeni na mikutano yote ya kisiasa.

Wagombea wanne wa urais nchini Kenya wametoa mipangilio ya mikutano yao ya mwisho ya kampeni za siasa. Kura za maoni zimeonyesha kwamba wapiga kura ambao hawajaamua mgombea wa urais watakayemchagua ni kati ya asilimia 6 hadi 8 ya walipiga kura walioandikishwa.

Akizungumza na kituo kimoja cha runinga Kenya, mtafiti na mchambuzi wa kura za maoni Tom Wolf, ameeleza kwamba katika muda huu mfupi uliosalia, wagombea wanazingatia maeneo waliko na ushawishi mkubwa, na palipo na wapiga kura wengi.

Mmoja wa wagombea urais wa Kenya, George Wajackoyah wa chama cha Roots, akiwa na mgombea mwenza Justina WamaePicha: Yasuyoshi Chiba/AFP

''Kunaweza kuwa na eneo nchini ambapo una uungwaji mkono mkubwa lakini hakuna wapiga kura wengi. Kwa hivyo unataka kuwekeza haya masaa na siku muhimu zilizosalia katika maeneo ambapo kuna wapiga kura wengi. Na labda pia kuangalia data ya namna watu walipiga kura katika chaguzi tatu ama nne zilizopita,'' alifafanua Wolf.

Ruto kurejea Nakuru

Naibu Rais William Ruto anatarajiwa kurejea jijini Nakuru Ijumaa baada ya kukamilisha mikutano katika maeneo ya Mlima Kenya ya Laikipia na Nyandarua. Muungano wake wa Kenya Kwanza unatarajiwa kukamilisha kampeni zake hapo Jumamosi mjini Narok na Nairobi. Aliyekuwa makamu wa Rais Musalia Mudavadi ambaye pia ni mfuasi wake ameelezea imani kuhusu matokeo mazuri kwenye uchaguzi wa wiki ijayo.

Kiongozi wa Muungano wa Azimio la Umoja Raila Odinga, anatarajiwa kufanya mikutano ya kampeni maeneo ya Lamu, Malindi na Mombasa. Na kuhitimisha kampeni zake jijini Nairobi alikopangiwa kufanya mkutano wa kisiasa katika uwanja wa Kasarani. Akizungumza katika eneo la Nyanza linaloaminika kuwa ngome yake, Raila amewataka wapiga kura kujitokeza kwa wingi.

David Mwaure, mgombea urais kupitia chama cha AganoPicha: Thomas Mukoya/REUTERS

''Nimekuja hapa leo, kuwaambia nyinyi watu wangu ya kwamba ninataka mjitokeze kwa kiwango cha asilia 100 wakati huu. Tusipoteze hata kura moja. Walio wagonjwa hospitalini nendeni mkawachukue wapelekeni wapige kura kisha muwarejeshe kwenye wodi. Walio na ulemavu wasaidiwe wapige kura, hakuna kulala,'' alisisitiza Raila.

George Wajackoyah mgombea wa urais kupitia tiketi ya chama cha Roots amepangiwa kufanya kampeni yake eneo la magharibi na kumalizia mikutano yake jijini Nairobi. Naye David Mwaure mgombea wa chama cha Agano atahitimishia mikutano yake Ijumaa na Jumamosi jijini Nairobi.

Kulingana na tume ya IEBC waliosajiliwa kupiga kura ni watu milioni 22, na 122,532, ambao ni pamoja na idadi ya wapiga kura 10,443 walio ughaibuni.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW