Kampeni za uchaguzi nchini Kongo kukamilika Jumatatu
18 Desemba 2023Human Rights Watch imetoa wito kwa mamlaka za Kongo kuchunguza haraka na bila upendeleo matukio ya vurugu yanayohusiana na uchaguzi na kuwashtaki waliohusika, bila ya kujali wanaegemea upande gani wa kisiasa.
Mtafiti mkuu wa Human Rights Watch tawi la Kongo Thomas Fessy ameeleza kuwa, shirika hilo limeorodesha matukio kadhaa ya vurugu kote nchini humo kati ya wafuasi wa vyama hasimu vya kisiasa ambayo yamesababisha mashambulizi ya kulipa kisasi, unyanyasaji wa kingono na kifo cha mtu mmoja.
Soma pia: Matamshi ya Cornelle Nangaa yaibuwa malumbano kati ya Kenya na DRC
Inaelezwa kuwa, zaidi ya watu milioni 1.5 hawataweza kushiriki zoezi la kupiga kura katika maeneo yenye mizozo, hasa katika jimbo la Kivu Kaskazini na jimbo la magharibi la Mai-Ndombe.
Pia mamilioni ya wakimbizi wa ndani pia huenda wasishiriki zoezi hilo.
Wachambuzi: Ushindani ni kati ya Tshisekedi na Moise Katumbi
Upinzani umeonyesha wasiwasi wao juu ya udanganyifu katika kura huku wakiishtumu serikali kwa kula njama na tume ya uchaguzi CENI na mahakama ya katiba, ambayo ndio msuluhishi wa mwisho wa migogoro ya uchaguzi.
Vyama vya upinzani na waangalizi wa uchaguzi mkuu huo wameonya kuwa baadhi ya kasoro zinatishia uhalali wa matokeo yatakayotangazwa. Miongoni mwa hizo ni kadi za wapiga kura zisizosomeka, kuzuiwa kwa ndege za baadhi ya wagombea wakati wa kampeni na kucheleweshwa kwa orodha za wapiga kura.
Soma pia: Mashambulizi ya mitandaoni kwa wagombea urais Kongo
Wachambuzi wanasema, huenda kusitokee machafuko iwapo matokeo rasmi yatalingana na yale ya waangalizi.
Siku tatu kabla ya kura, wagombea 19 wako kwenye orodha ya kuwania urais.
Kutokana na wasiwasi juu ya uaminifu wa uchaguzi huo, baadhi ya waangalizi wanaamini kuwa Rais wa sasa Felix Tshisekedi na Moise Katumbi ndio washindani wakuu kutokana na raslimali zao na ufuasi mkubwa walio nao kwenye mikutano ya kampeni.
Pia, kutokana na mgawanyiko wa upinzani, Tshisekedi anaonekana kuwa na nafasi nzuri ya kushinda.