1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa zaanza Tanzania

20 Novemba 2024

Kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa zimeanza leo Tanzania huku vyama vya upinzani vikiapa kutosusia uchaguzi huo licha ya idadi kubwa ya wagombea wa vyama hivyo kuenguliwa wakidaiwa kutokuwa na sifa za kugombea.

Tanzania | Uchaguzi | Dar es Salaam
Wapiga kura nchini Tanzania wakisubiri kuandikishwa kwa uchaguzi wa serikali za mitaa Picha: Florence Majani

Chama tawala cha CCM kimesambaza viongozi wake wakuu katika mikoa mbalimbali kuzindua kampeni zao leo huku wapinzani, ACT-Wazalendo na Chadema nao wakinoa wembe ule ule.

Licha ya kulia rafu hasa katika mchakato wa uteuzi wa wagombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa, vyama vya upinzani katika taifa hili la Afrika Mashariki, vimejinasibu kufanya kampeni nchi nzima.

Vyama vya upinzani ACT -Wazalendo na Chadema vimesema pamoja na idadi kubwa ya wagombea wao kuenguliwa wakidaiwa kukosa sifa za kugombea, lakini vimejipanga kufanya kampeni nchi nzima.

Soma pia: Mbowe: Mifarakano ya CHADEMA ni jambo la kawaida 

Akizungumza na DW, Kiongozi Mkuu wa ACT-Wazalendo Dorothy Semu amesema chama hicho kitapita nchi nzima kunadi sera na ilani yake hata kama kina idadi ndogo ya wagombea.

ACT kimesema Kiongozi wa Chama mstaafu, Zitto Kabwe, Mwenyekiti wa Ngome ya Wanawake, Janeth Rithe na Mwenyekiti wa Ngome ya Vijana, Abdul Nondo wataongoza kampeni za viongozi wa kitaifa mikoa ya Tabora, Katavi, Rukwa na Tabora. 

"Karibu watu 51, 000 wameondolewa viongozi wa nafasi mbalimbali sisi tumeamua kwenda na hawa wachache waliobaki kwenye maeneo ya nchi nzima kuwanadi, na kuhakikisha wanashinda na wanatumia muongozo wa ilani ya ACT- kunadi sera zetu na kuwashawishi wananchi," amesema Zitto Kabwe.

Chadema kufanya kampeni nchi nzima

Makamu mwenyekiti wa Chadema Tanzania Bara Tundu LissuPicha: AP Photo/picture alliance

Kama ilivyo kwa ACT-Wazalendo, CHADEMA wamesema watafanya kampeni zao nchi nzima ambapo Makamu Mwenyekiti wa chama hicho -Bara, Tundu Lissu, leo anazindua kampeni wilaya ya Ikungi, Singida na viongozi wengine wakuu wa chama hicho wanatarajiwa kuzindua kampeni kuanzia kesho.

Mkurugenzi wa Itikadi, Mafunzi na Mawasiliano, John Mrema amesema, "Dar es Salaam kwa leo wanafanya wenyeji,viongozi wakuu ratiba zao zinaanza kesho isipokuwa ratiba kwa Makamu mwenyekiti ambaye ameanzia Singida wengine ratiba zao zinaanzia kesho, tutafanya mikutano ya hadhara."

Chama tawala cha CCM kimesambaza viongozi wake wakuu, ambao kimsingi ndiyo wajumbe wa kamati kuu ya chama hicho katika mikoa mbalimbali kwa minajili ya kuzindua kampeni.

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango atazindua kampeni Dodoma, Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko atazindua kampeni Mara, Waziri Mkuu Kassim majaliwa amezindua kampeni mkoa wa Kigoma na Spika wa Bunge Tulia Ackson yeye akitarajiwa kuzindua kampeni mkoa wa Songwe.

Soma pia: CHADEMA yamjibu Lissu, makada wake kuhusu madai ya rushwa 

Akizindua kampeni mkoani Mbeya, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Bara, John Mongela amesema siku saba za kampeni kwa CCM, ni siku saba za moto.

"Kwamba tarehe 20 leo nchi nzima kampeni za serikali za mitaa kama ratiba zilizotolewa na Tamisemi zianze, wajumbe wa halmashauri kuu wapo mikoani, kwa ajili ya kuzindua kampeni, hii kampeni tunaiita siku saba za moto."

Kwa mujibu wa Wizara inayosimamia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI),kati ya  nafasi 80,430 zinazogombewa katika uchaguzi huo,

CCM imeweka wagombea katika nafasi zote huku vyama vingine 18 vya siasa vikiweka wagombea katika nafasi 30,977 sawa na asilimia 38.51.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW