1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za uchaguzi zaanza rasmi nchini Burundi

Amida Issa27 Aprili 2020

Kampeni za uchaguzi wa urais utakaofanyika Mei 20 zimeanza leo nchini Burundi ambapo mgombea urais kupitia chama tawala CNND-FDD, Evariste Ndayishimiyena na Agathon Rwasa wa chama cha upinzani, CNL wamezindua kampeni zao

Afrika Wahl in Burundi
Picha: Reuters/M. Hutchings

Mkuu wa Tume ya Uchaguzi, Pierre Claver Kazihise, amewaonya vikali wale wote watakaokwenda kinyume na sheria, huku waziri wa afya akiwakumbusha wagombea na raia kuzingatia kanuni za kuepukana na ugonjwa wa COVID-19. 

Ni katika tarafa ya Bugendana mkoani Gitega kati mwa nchi, ndiko Evariste Ndayishimiye mgombea wa chama cha CNDD-FDD alikoanzia kampeni akiwa pamoja na vigogo wa chama hicho, akihudhuria pia Rais Pierre Nkurunziza, mwenye cheo cha kiongozi wa milele wa chama hicho.

Wafuasi wa chama wameonekana wakivalia sare za chama hicho zilochapishwa: Tumpigiye kura Evariste Ndayishimiye."

Mgombea urais kupitia chama tawala CNND-FDD Evariste NdayishimiyePicha: Reuters/E. Ngendakumana

Mgombea huyo wa chama tawala tayari amepata uungaji mkono kutoka vyama vya FNL kinachoongozwa na Jaques Bigirimana, muungano wa COPA, na wafuasi wa UPRONA wanaoelemea kundi la Isidore Mbayahaga.

Naye muwania kiti cha urais kwa tikiti ya chama cha upinzani cha CNL, Agathon Rwasa, amezindua kampeni yake katika mkoa wa Ngozi alikozaliwa, walikojumuika wafuasi wake kutoka mikoa ya kaskazini mwa nchi.

Kampeni yake imetanguliwa na gwaride lilotajwa kuwa la amani, kabla ya kujumuika kwenye uwanja wa michezo Muremera.

Mgombea wa chama cha upinzani azindua kampeni yake katika mkoa alikozaliwa

Agathon Rwasa wa chama mashuhuri cha upinzani CNLPicha: Getty Images/AFP/C.de Souza

Terence Manirambona msemaji wa chama chama hicho akisema wanaingia katika kampeni wakiwa na malalamiko kadhaa na kwamba wafuasi wao wanaendelea kunyanyaswa. Lakini lazima mambo yabadilike. Amesema "Tumewataka wafuasi wetu kutonaswa kwenye mitego ya wanaowachokoza, na baadaye kujikuta wakifungwa. Matukio tuliyonayo ni mengi . Lazima twende kwenye uchaguzi hali hiyo iweze kubadilika."

Naye Gaston Sindimwo, makamu wa kwanza wa rais aliyesusiwa na baadhi ya wafuasi wa chama chake Uprona ameendesha kampeni katika mkoa wa Mwaro, huku Domitien Ndayizeye, mgombea wa muungano wa vyama Kira Bdi akiwa katika mkoa wa Muramvya katikati mwa nchi.

Leonce Ngendakumana muwania kiti cha urais kwa tikiti ya chama Sahwanya Frodebu, ameendesha kampeni yake katika kata ya Kinama kaskazini mwa Bujumbura.

Hayo yakijiri, mkuu wa Tume ya Uchaguzi - CENI - Pierre Claver Kazihise, amewaonya wagombea watakaokwenda kinyume na sheria ya uchaguzi kwa kusema "Kwa upande wake, Waziri wa Usalama Alain Guillaume Bunyone amewataka wagombea kujiepusha na kauli za uchokozi zinazoweza kuhatarisha usalama, huku Waziri wa Afya Thadee Ndikumana akiwataka wagombea na raia kuzingatia kanuni za kujikinga na janga la kirusi cha corona."

Kampeni hii iloanza leo itamalizika Mei 17 siku 3 kabla ya uchaguzi utakaofanyika Mei 20. Wagombea 7 kiti cha urais wameorodheshwa na CENI, ambapo mgombea wa chama tawala, Evariste Ndayishimiye, na yule wa chama cha upinzani cha CNL, Agathon Rwasa, wakitabiriwa kuchuwana vikali.

 

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi

Gundua zaidi