1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za uchaguzi zahitimishwa Tanzania

28 Oktoba 2025

Kampeni za uchaguzi mkuu nchini Tanzania zinafungwa rasmi siku ya Jumanne (28.10.2025) huku wagombea wa urais, wagombea wenza pamoja na wafuasi wao wakiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Uchaguzi Tanzania I Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Samia Suluhu Hassan
Rais wa Tanzania na Mgombea wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Samia Suluhu HassanPicha: CCM

Wagombea kutoka vyama 17 vinavyoshiriki uchaguzi huo Jumanne hii wanatupa karata zao za mwisho kwa wapiga kura kabla ya hatma yao kuamuliwa wakati wapiga kura wenyewe watapoanza kuteremka katika vituo vya kupigia kura siku ya Jumatano.

Siku 61 za kampeni zimeshuhudia wagombea kuanzia ngazi ya udiwani, ubunge na urais wakizunguka maeneo mbalimbali ya nchi wakiwarai wapiga kura kuwapeleka katika usukani wa madaraka ili kutekeleza kile walichokiahidi.

Hata hivyo, ingawa uchaguzi huu unashuhudia wagombea 17 wakiwa katika makabrasha ya kupigiwa kura, lakini wadadisi wa mambo wanakitazama chama tawala cha CCM ndicho kilichotawala zaidi majukwaa ya kampeni.

Umahiri wake katika siasa za Tanzania, nguvu za kifedha katika kuendesha kampeni pamoja na kujiweka kando kwa chama kikuu cha upinzani CHADEMA, kumeifanya CCM kuwa na uwanja mpana zaidi kwa kutawala majukwaa wakati wote wa kampeni.

Kiongozi wa chama kikuu cha upinzani Tanzania CHADEMA, Tundu Lissu ambaye chama chake kimesusia uchaguzi kikidai kufanyike mageuzi kwenye mfumo mzima wa uchaguziPicha: Ericky Boniphace/DW

Baadhi ya  vyama vya upinzani  ambavyo vinashiriki uchaguzi huu kwa nyakati fulani vimearifiwa kuendesha kampeni kwa kusua sua kutokana na kukabiliwa na ukata wa fedha. Hata hivyo vyama vyote hivyo leo viko majukwaani vikihitimisha kampeni zake. Wakati huu chama tawala CCM kimewakusanya wanachama wake katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza kwa ajili ya kuhitimisha kampeni zake ambako mgombea wake, Rais Samia Suluhu Hassan atanadi sera zake katika dakika za lala salama.

Mwenyekiti wa umoja wa vijana wa CCM, Ally Mohammed Kawaida amesema kundi la vijana ni moja ya tegemeo la chama hicho katika uchaguzi huu:

" Na leo nataka nimwage ugali ndugu mwenyekiti, kampeni zako za uchaguzi zilikuwa zikiwashirikisha vijana wa chama cha mapinduzi na wasio wa chama cha mapinduzi."

Ama uchaguzi wa mwaka huu umegubikwa na kile kinachotazamwa kama ukosoaji wa mitandaoni ambako wananchi wa ndani na wale wa nje ya nchi wamekuwa wakitumia majukwaa hayo kwa ajili ya kujadili na kuhamasisha maandamano.

Onyo la Polisi kuhusu kuzusha vurugu

Jeshi la Polisi limeonya kuhusu hatua yoyote itakayoweza kutibua uchaguzi huo na kusema kwamba linakusudia kufanya doria karibu maeneo yote ya nchi. Msemaji wa Jeshi la Polisi Tanzania , David Misime ametoa msimamo wa jeshi hilo kuelekea uchaguzi huo:

" Atakayedhubutu kuvunja sheria asilaumu kwa hatua zitakazochukuliwa dhidi yake kwa mujibu wa sheria."

Polisi wa Tanzania wakiwa kwenye doria jijini Dar Es salaamPicha: Ericky Boniphace/DW

Kando na hilo, baadhi ya makomandoo wa polisi mikoani wanasema tayari wamefunga kamera maalumu mitaani zitakazotumika kwa ajili ya kuimarisha doria. Wakuu wa mikoa na wilaya pia wamekuwa wakiwaonya wananchi.

Kwa upande mwingine baadhi ya wagombea wa vyama vya upinzani wanalalamika kuhusu mawakala kufanyiwa mizengwe kwa kunyimwa fursa ya kuapishwa hali ambayo inawanyima uhalali wa kusimamia uchaguzi:

" Mimi mgombea ubunge jimbo la Kibamba kupitia chama cha Ukombozi wa Umma (Chauma) wasimamizi wasaidizi walituhujumu makala wengi wa Chauma hawakuapishwa."

Tume Huru ya Taifa ya  Uchaguzi , INEC inasema maandalizi kwa ajili ya uchaguzi huo wa rais, wabunge na madiwani yamekamilika na wengi sasa wanasubiri kuona hali itakavyokuwa siku ya Jumatano.

Wakati huo huo baadhi ya wamiliki wa vyombo vya usafiri wa nchi kavu kama vile Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania, TABOA, na usafiri wa majini vimetangaza kusitisha huduma za usafiri siku ya upigaji kura, ili kupisha uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, na kutoa nafasi kwa wananchi kushiriki kikamilifu kwenda vituoni kupiga kura.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW