1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUturuki

Kampeni za uchaguzi zapamba moto nchini Uturuki

8 Mei 2023

Wiki moja kabla ya uchaguzi mkuu nchini Uturuki, muungano wa vyama sita vya upinzani ulifanya kampeni na kuwahutubia maelfu ya wafuasi katika mkutano wa hadhara mjini Istanbul mwishoni mwa juma lililopita.

Türkei Istanbul Wahlen Präsident Recep Tayyip Erdogan
Picha: Umit Bektas/REUTERS

Kemal Kiliçdaroglu, ni mpinzani na mgombea urais ambaye kura za maoni zinamuonyesha akiwa mbele kidogo ya rais anayemaliza muda wake nchini Uturuki Recep Tayyip Erdogan.

Jumamosi iliyopita, Kemal Kiliçdaroglu aliuambia umati uliyokuwepo katika wilaya ya Maltepe ya Istanbul kwamba utakuwa na fursa ya kuubadili utawala wa kimabavu kupitia mfumo wa kidemokrasia na kusisitiza kuwa mabadiliko ya serikali ya kidemokrasia nchini Uturuki itakuwa zawadi kwa ulimwengu wa kisiasa.

Ama kuhusu utawala wa Rais Erdogan, Kiliçdaroglu alisema hawatoiacha Jamhuri ya Uturuki mikononi mwa mtu mmoja akiahidi kurejesha utawala wa sheria na haki. Katika historia ya Uturuki, mikutano ya kampeni mjini Istanbul kwa jadi huwa mingi na mikubwa zaidi.

Soma pia: Uturuki yawakamata watu 110 kwa madai ya kigaidi

Wafuasi wa rais wa sasa wa Uturuki Tayyip Erdogan wakihudhuria Kampeni ya uchaguzi 07.05.2023 mjini Istanbul.Picha: Umit Bektas/REUTERS

Erdogan ambaye katika uchaguzi huu anakabiliwa na changamoto kubwa zaidi kwa miongo miwili, aliwakusanya pia siku ya Jumapili wafuasi wake mjini Istanbul, huku kukiwa na mgogoro wa kiuchumi kutokana na tetemeko la ardhi la mwezi Februari mashariki mwa Uturuki ambalo lilisababisha vifo vya watu zaidi ya 50,000.

Kampeni za uchaguzi nchini Uturuki zimepamba moto kabla ya uchaguzi mkuu wa rais na wabunge utakaofanyika Mei 14 huku marudio yakitarajiwa Mei 28. Erdogan amekuwa akiwashutumu wabunge wa upinzani kwa vitendo vya uhaini na kuunga mkono ugaidi.

Kampeni za Erdogan kupambana na upinzani

Siku ya Jumamosi, Erdogan alikuwa katika mji wa kusini wa Mersin ambako alielezea uchaguzi huo kama zoezi la kujinusuru dhidi ya wale anaowaita "magaidi," huku akitaja madai ya uhusiano kati ya mgombea mkuu wa upinzani Kiliçdaroglu na Chama cha Wafanyakazi wa Kikurdi kilichopigwa marufuku cha PKK.

Upinzani, ambao unakanusha shutuma hizo, ulitowa wito wa utulivu na kudai mwishoni mwa juma kuwa timu ya Erdogan inajiandaa kuanza vita vya mtandaoni ili kumdhalilisha Kiliçdaroglu, kwa kutumia video au sauti bandia.

Soma pia: Upinzani wa Uturuki kusambaza waangalizi 500,000 uchaguzi wa Mei 14

Katika kukabiliana na upotoshaji huo unaoweza kutokea, msaidizi wa Kiliçdaroglu Engin Özkoç amesema wanajiandaa kutumia mbinu ya kutambua na kufichua taarifa na vyanzo bandia, huku Mkurugenzi wa mawasiliano wa Erdogan Fahrettin Altun akitupilia mbali madai hayo ya mapambano ya mtandaoni na kusema ni uongo mtupu.

Rais wa Uturuki Tayyip ErdoganPicha: Umit Bektas/REUTERS

Waziri wa sheria wa Uturuki amesema leo kuwa zaidi ya watu kumi na wawili wamezuiliwa kufuatia ghasia zilizozuka kwenye mkutano wa kampeni za upinzani mashariki mwa Uturuki katika mji wa Erzurum mwishoni mwa juma.

Meya wa Istanbul Ekrem Imamoglu kutoka chama kikuu cha upinzani cha Republican People's Party, CHP, wakati akihutubia akiwa kwenye basi la kampeni Jumapili alasiri, alishambuliwa na kundi kubwa la waandamanaji wapatao takriban 200 na ambao walianza kumrushia mawe. Imamoglu alikuwa akifanya kampeni kwa niaba ya kiongozi wa CHP na mgombea urais Kemal Kilicdaroglu, na ambaye ndiye mpinzani mkuu wa Rais wa sasa wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan.

 

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW