1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za urais zaanza DRC

Benjamin Kasembe22 Novemba 2018

Kampeni za uchaguzi wa rais katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo zimeanza rasmi. Uchaguzi mkuu unatarajiwa Disemba 23.

Kongo Emmanuel Ramazani Shadary
Picha: REUTERS

Picha za wagombea zimeanza kuonekana kila sehemu hasa katika maeneo ya umma katika mji wa Goma ikitowa ishara tosha kwamba uzinduzi rasmi wa kampeni ya uchaguzi mkuu nchini Kongo umeanza.

Hali ya usalama katika miji mikuu ikiwa inaonekana kuimarika; maeneo ya vijijini bado makundi ya wapiganaji yenye kumiliki silaha yanaendelea kushamiri katika misitu. Hii ni licha ya operesheni za kijeshi zinazoendeshwa na jeshi tiifu kwa serikali ya CONGO. Wakati huo huo wagombea wanawake katika uchaguzi wanaoishi kwenye maeneo yanayokumbwa na migogoro wamelalamika kuwa na uwoga wa kuendesha harakati zao za Kampeini, kufuatia usalama mdogo, utekwaji nyara wa raia na vitendo vya ubakaji dhidi ya wanawake.  

Akizungumza na DW Sharrifa Mulyata mgombea wa nafasi ya ubunge katika eneo la Rutshuru ameitaka serikali kuwalindia usalama katika kipindi hiki cha uchaguzi

Kwa ujumla ni wagombea 85 wanawake wanaotoka Kivu ya kaskazini, jimbo ambalo kwa miongo kadhaa linakabiliwa na vita vinavyoendeshwa na makundi ya majimaji huku ikipelekea wanawake wengi kukata tamaa ya kuingia katika siasa. Upande wake Melanie Mahamba ambaye ni mwanachama wa chama tawala hapa kivu kaskazini amesema kwamba wanawake wako tayari kunyakua ushindi katika uchaguzi mkuu.

Kuanzishwa kwa kampeni hii ya uchaguzi nchini DRC, kunajiri wakati ambapo maeneo mengi hapa mashariki mwa DRC yamekuwa na uhaba wa barabara na kuongezeka kwa makundi ya waasi wa majimaji wanaoendesha mashambulizi dhidi ya vijiji vya raia hasa katika mitaa ya Beni, Rutshuru, Masisi na Lubero; maeneo ambayo hadi sasa operesheni za kuvisaka vikundi hivyo zaendeshwa na jeshi wa FARDC.

Wanawake wanaoegemea upinzani wamesema kwamba licha ya upinzani kugawanyika wao,wataendelea kusimama imara ili kunyakua ushindi katika uchaguzi mkuu.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW