1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampeni za urais zang'oa nanga Uganda

Lubega Emmanuel9 Novemba 2020

Wagombea urais 11 nchini Uganda wameanza rasmi kampeni ambazo zitadumu kwa siku 63, kuelekea uchaguzi mkuu mwakani. Hayo yakijiri, polisi wamesisitiza kuwa ni sharti kanuni za kudhibiti COVID-19 zifuatwe.

Bildkombo Yoweri Museveni und Bobi Wine

Wagombea urais 11 nchini Uganda leo wameanza rasmi harakati za kusaka kura kutoka kwa wananchi. Kipindi hicho cha siku 63 kimebashiriwa kuwa kigumu kwa wagombea wa upinzani hasa wale ambao watakaidi kanuni za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19 kwani polisi wanasisitiza kanuni hizo zifuatwe na kila mtu.

Hali hii imeshuhudiwa hii leo wakati baadhi ya wagombea na wafuasi wao walipokabiliana na polisi sehemu mbalimbali za nchi. 

Soma pia: Wagombea urais Uganda wazindua ilani zao

Hao ni wafuasi wa chama cha FDC wakikabiliana na polisi mjini Jinja Mashariki mwa Uganda wakati mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho Patrick Oboi Amuriat maarufu kama POA alipokuwa akijiandaa kuelekea mji wa Soroti ambapo angezidua kampeni zake.

Mgombea huyo ambaye amechukua mahala pa Dr. Kizza Besigye katika kupeperusha bendera ya chama hicho kikuu cha siasa upande wa upinzani ameapa kuhakikisha kuwa atakaidi baadhi ya kanuni za kudhibiti ugonjwa wa COVID-19 anazoelezea kuwa kisingizio cha polisi kunyanyasa upinzani.

Dr. Kizza BesigyePicha: DW/E. Lubega

Hata hivyo jeshi la polisi limesisitiza kuwa limejiandaa kukabiliana na yeyote atakayevunja kanuni zilizowekwa kudhibiti ugonjwa wa COVID-19 katika kipindi hiki cha siku 63 za kampeni za urais na ubunge. Miongoni mwa kanuni hizo ni kuwa na watu wasiozidi 70 katika vikao vya mikutano wakiwa wamevalia barakoa.

Chama cha NUP kwa upande wake hakikuweza kuanza kampeni zake za kusaka kura za mgombea wao Robert Kyagulanyibaada ya kuibuka mgongano kwenye ratiba na chama tawala cha NRM.

Vyama vyote viwili vilitaka kuanzia kanda ya Kati mwa nchi lakini NRM kikapewa nafasi hizo. Katibu mkuu wa NRM Kasule Lumumba amelezea kuwa ni jadi yao kuanzia kanda ya Luwero ambako rais Museveni alianzisha harakati zilizomfikisha madarakani mwaka 1986.

Katika kikao cha wanahabari mgombea wa NUP ambacho vuguvugu lake ni People power Bobi amefafanua hivi kuhusu mikakati yake ikiwa atachaguliwa kuwa rais.

Tume ya uchaguzi ilitangaza tarehe 14 Januari mwakani 2021 kuwa siku ya uchaguzi mkuu. 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW