1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kampuni la ulinzi lahusika na mauwaji nchini Irak

Oummilkheir18 Septemba 2007

Blackwater latakiwe lisitishe shughuli zake nchini Irak

Watumishi wa kampuni la Blackwater nchini Irak
Watumishi wa kampuni la Blackwater nchini IrakPicha: AP

Serikali ya Irak imelipokonya liseni kampuni la ulinzi la kimarekani-Blackwater-linalotuhumiwa kuhusika na tukio lililogharimu maisha ya wairak wanane.Waziri wa mambo nya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice “ameomba radhi”.

Serikali ya Irak inapanga kuwafikisha mahakamani watumishi wa kampuni hilo wanaohusika na kisa hicho.Jaji mmoja wa mahakama kuu ya sheria nchini Irak,Abdel Sattar Ghafour Bairaqdar amesema kampuni hilo na watumishi wake wanaweza kuhukumiwa kuambatana na sheria za Irak..

Msemaji wa wizara ya ndani amesema walinzi wanaolitumikia kampuni la Blackwater,kampuni mojawapo kati ya makampuni makubwa ya kibinafsi yanayosimamia usalama wa wanadiplomasia wa kimarekani nchini Irak,walifyetua risasi baada ya mzinga kuporomoshwa karibu na magari yao katika mtaa wa Mansour,magharibi ya Baghdad.

“Watumishi wa Blackwater walifyetua ovyo risasi dhidi ya wapiti njia”-amesema hayo jenerali Abdulkarim Khalaf-aliyezungumzia hapo awali juu ya kuuliwa watu 11 ,akiwemo polisi mmoja na watu wengine 13 kujeruhiwa.

Jenerali Abdulkarim Khalaf hakufafanua watumishi wangapi wa Blackwater wanahusika na kisa hicho.Amesema tuu wachunguzi wamefika mahala kisa hicho kilikotokea na kuna mashahidi.Wachunguzi hao wameelekea hivi sasa katika makao makuu ya Blackwater mjini Baghdad

Msemaji wa wizara ya mambo ya nchi za nje ya Marekani Sean McCormack anasema:

“Uchunguzi unasendelea.Idara ya usalama ya ubalozi wetu inasimamia uchunguzi huo.Makampuni mengine kadhaa ya kimataifa yanashirikiana na idara yetu.Kwa hivyo bado ni mapema kutamka lolote kuhusiana na kisa hicho.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleezza Rice amezungumza kwa simu jana usiku pamoja na waziri mkuu Nuri el Maliki na kuelezea masikitiko yake kutokana na kuuliwa watu wasiokua na hatia.Mwanadiplomasia huyo amehakikisha Marekani itafanya kila liwezekanalo kuzuwia kisa kama hichoi kisitokee siku za mbele.

Ubalozi wa Marekani mjini Baghdad umedhibitisha wanashirikiana na serikali ya Irak kuchunguza kisa hicho,lakini hawakutaka kudhibitisha kama kampuni la Blackwater limepokonywa liseni.

Kampuni hilo linadai halijapokea bado amri ya kutoendesha shughuli zake nchini Irak.

Baraza la wawakilishi la Marekani linapanga kujadili kisa hicho.

Mkuu wa chama cha itikadi kali cha washiya,Moqtadar el Sadr anataka makampuni yote ya kigeni yanayofanya kazi nchini Irak,yapigwe marufuku.

Muqtadar el Sadr anataka wahusika waandamwe kisheria na wahanga walipwe fidia.