Kampuni ya tumbaku ya BAT yatuhumiwa kwa rushwa Afrika
24 Agosti 2017Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa hii leo na gazeti la Guardian, kampuni ya British American Tobacco (BAT) imekuwa ikikabiliwa na tuhuma kadhaa za kujihusisha na matumizi ya rushwa barani Afrika ili kujinufaisha na biashara ya uuzaji sigara dhidi ya washindani wake kibiashara na kukwamisha juhudi za serikali katika kuzuia uvutaji sigara barani humo.
Mapema mwezi huu, taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa ya nchini Uingereza ya Serious Fraud Office (SFO) ilianzisha uchunguzi dhidi ya kampuni ya BAT kuhusiana na tuhuma hizo.
Taarifa ya uchunguzi iliyochapishwa na gazeti la Guardian la tarehe 18 Agosti 2017 ilifichua madai mapya kuwa kampuni ya BAT kwa miaka kadhaa imekuwa ikipenyeza mamilioni ya dola za kimarekani kwa njia ya siri na kinyume cha sheria kwa kampuni inayohusika na uzalishaji pamoja na usindikaji wa tumbaku katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa lengo la kuisaidia shughuli za kampuni hiyo hiyo nchini humo.
Tuhuma hizo mpya zinaonesha kuwa kampuni ya BAT kwa miaka mingi imekuwa ikiwatumia waasi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kupenyeza pesa kwa njia za siri kwa wakulima wa tumbaku katika eneo la Auzi nchini humo.
Aidha ripoti hiyo inaibua maswali iwapo BAT pia inakiuka sheria dhidi ya matumizi ya fedha chafu hasa ukichukulia ukweli kwamba Marekani ilikuwa imeiwekea vikwazo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwaka 2006.
BAT yatuhumiwa kusambaza sigara zisizo na ubora Sudan Kusini
Mbali na hayo, BAT inatuhumiwa kusambaza sigara zisizo katika kiwango cha ubora unaotakiwa nchini Sudan Kusini hususani katika kipindi hiki ambacho taifa hilo changa barani Afrika linakabiliwa na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe, huku pia ikishirikiana na mitandao ya kigaidi nchini Somalia kwa lengo la kuendeleza mauzo ya sigara nchini humo.
Tuhuma hizi zimeibuka upya hasa baada ya kampuni ya BAT kuungana na kampuni ya Reynolds ya Marekani mnamo Julai 2017 ambapo kwa mujibu wa kampuni hiyo hatua hiyo imeiwezesha kuwa kampuni kubwa na inayotengeneza faida kubwa katika biashara ya tumbaku duniani.
Metthew L. Meyer ambaye ni rais wa taasisi inayohusika na kampeni dhidi ya kuzuia matumizi ya tumbaku kwa watoto ya Tobacco Free Kids amesema kulingana na historia ya muda mrefu inayoihusu kampuni ya BAT ndani ya Marekani na nje ya nchi hiyo kwa ujumla tuhuma zinazoikabili lazima zichunguzwe kwa kina na vyombo vinavyohusika.
Amesema kampuni hii inaonesha kuwa haiwezi kufuata sheria hadi pale itakapowajibishwa na serikali husika, washika dau, na washirika wa biashara kwa ujumla ndipo inaweza kuachana na mwenendo huo.
Matumizi ya tumbaku yanakisiwa kuua zaidi ya watu milioni saba kila mwaka duniani na huenda ikauwa kiasi cha watu bilioni moja katika karne hii.
Mwandishi: Isaac Gamba/afpe
Mhariri: Mohammed Khelef