1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kane atetemesha Bundesliga

28 Agosti 2023

Mshambuliaji wa Bayern Munich Harry Kane anasema wiki iliyopita ilikuwa njema kwake kwani mkewe alijifungua na Jumapili akafunga magoli 2 na kuisaidia timu yake ya Bayern kupata ushindi wa 3-1 dhidi ya Augsburg.

Bundesliga Bayern Munich - FC Augsburg
Mshambuliaji wa Bayern Munich Harry Kane baada ya kufunga dhidi ya AugsburgPicha: Tom Weller/dpa/picture alliance

Hiyo ilikuwa mechi yake ya kwanza ya Bundesliga katika uwanja wa nyumbani wa mabingwa hao wa Ujerumani, Allianz Arena.

Kwa ujumla sasa Kane amefunga magoli 3 katika mechi mbili alizoichezea Bayern tangu ajiunge nao.

"Unajua mara tu nilipojiunga na timu hii, nilitaka kusaidia kwa kila namna na kufunga mabao ndio sababu kuu ya uwepo wangu hapa. Nafurahi kufunga magoli leo na nilikuwa na nafasi nyengine nzuri ambayo ningefunga ila yote tisa, nafurahi kwa matokeo na pia mchango wangu," alisema Kane.

Wachezaji wa Bayern Munich wakisherehekea goli dhidi ya AugsburgPicha: Ulrich Gamel/kolbert-press/IMAGO

Kocha wake Thomas Tuchel lakini anahisi kwamba bado bayern haijamtumia Kane vyema kwani ana matumaini makubwa kwamba ana uwezo wa kufunga mabao mengi zaidi.

"Nafikiri atakapocheza mechi nyingi na sisi tutampa pasi nyingi zaidi na nafikiri ataweza kufunga zaidi. ila unajua Harry ni mchezaji wa kulipwa na ni mshambuliaji mahiri kwa hiyo anajua kinachohitajika. Hana shinikizo," alisema Tuchel.

Bayern sasa wana pointi 6 kutokana na mechi zao mbili walizocheza ila mwishoni mwa wiki watakuwa na kazi ngumu kupambana na Borussia Mönchengladbach ambao kwa kawaida huwapa changamoto kila msimu wanapokumbana.

Vyanzo: Reuters/DPAE

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW