1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kane: Bayern itazidi kuimarika msimu unavyosonga

23 Oktoba 2023

Harry Kane alifunga goli lake la 9 katika Bundesliga msimu huu katika ushindi wa 3-1 wa Bayern Munich dhidi ya Mainz siku ya Jumamosi.

Fußball Bundesliga | 1. FSV Mainz 05 - FC Bayern München
Harry Kane akisherehekea goli lake na wachezaji wenzake wa Bayern MunichPicha: Arne Dedert/dpa/picture alliance

Ushindi wa Bayern uliwawekea shinikizo vinara wa ligi Bayer Leverkusen ambao wenyewe walipata ushindi wa 2-1 walipokuwa ugenini Wolfsburg.

Leverkusen, Bayern na Dortmund ndizo timu za pekee ambazo hazijapoteza mechi za ligi kufikia sasa baada ya Dortmund kuwazidi kete Werder Bremen moja bila siku ya Ijumaa.

Harry Kane kwa upande wake anasema anajihisi yuko imara kabisa na anatumai Bayern itakuwa timu bora zaidi kadri msimu unavyozidi kusonga.

"Jinsi tunavyocheza, wakati mwengine napenda kurudi nyuma na kusaidia kuwaandalia nafasi za kufunga kina Sane, Kingsley Coman na Jamal Musiala. Kwa hiyo nafikiri tunajuana vyema zaidi na nahisi kila wiki naendelea kujihisi nyumbani," alisema Kane.

Kuridhika na ushindi dhidi ya Mainz 05

Kocha wa Bayern Thomas Tuchel naye anasema ushindi walioupata dhidi ya Mainz haukuwa rahisi kwa kuwa timu yake ina wachezaji wengi ambao wanazichezea timu zao za taifa na ndio mwanzo wengine walikuwa wamerudi kutoka kwenye majukumu ya kimataifa.

Kocha wa Bayern Munich Thomas TuchelPicha: Benjamin Westhoff/REUTERS

"Ilikuwa ngumu kwetu na ndio maana naisifu timu yangu. Tuna watu kutoka Marekani, Korea Kusini, wachezaji waliokuwa wamerudi kutoka kwenye kuumwa kama Kimmich, de Ligt ndio alikuwa amerudi kutoka kwenye jeraha na sasa hivi Leon Goretzka amepata jeraha la mkono na alicheza akiwa na jeraha la kifundo cha mguu pia. Ni vigumu kuwazuia Mainz kwasababu wanapenda kucheza mchezo wa vurugu," alisema Tuchel.

Chanzo: AFPE/Reuters