1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kanisa Katoliki Kongo lamshutumu Tshisekedi

27 Juni 2023

Kanisa Katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo limeshutumu kile linachosema ni "matumizi mabaya ya vyombo vya sheria" yanayofanywa na serikali ya Rais Félix Tshisekedi.

Felix Tshisekedi Präsident DR Kongo
Picha: Isa Terli /AA/picture alliance

Miezi sita kabla ya uchaguzi mkuu hapa Kongo, kumeibuka mvutano mpya baina ya mamlaka ya Kinshasa na Kanisa Katoliki, baada ya maaskofu kuushutumu utawala wa Tshisekedi kwa utumiaji mbaya wa vyombo vya sheria pamoja na kuendesha vibaya mchakato wa uchaguzi.

Kauli hiyo inatanguliwa na ile ya Tshisekedi ambaye alitumia ziara yake katika ngome yake ya Mbujimayi mkoani Kasai Mashariki kushutumu kile alichokitaja kuwa ni "dhuluma katika Kanisa Katoliki."

Soma zaidi: Martin Fayulu awataka Bemba na Katumbi kuchukuwa maamuzi

"Labda hii ni fursa kwangu kukosoa mkurupuko fulani unaoonekana ndani ya Kanisa Katoliki. Mtafaruku ambao nauelezea kuwa hatari, hasa katika mwaka huu wa uchaguzi. Kanisa lazima liwe katikati ya kijiji." Alisema Tshisekedi.

Kanisa Katoliki lajibu

Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Muungano wa Makanisa nchini Kongo (CENCO), Askofu Donatien Tshole, alisema Kanisa Katoliki ndiyo madhehebu makubwa ya kidini, ambalo linaendelea kuwahudumia wanyonge na hata yeye "Rais Félix Tshisekedi alinufaika na huduma za kanisa hilo alipokuwa bado upande wa upinzani."

Waumini wa Kanisa Katoliki nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.Picha: Justin Makangara/REUTERS


"Anajua jinsi Kanisa linavyotumikia siku zote na alinufaika na huduma zile zile wakati Kanisa lilipokuwa likikumbusha kwa niaba yao wapinzani maadili ambayo hayakuheshimiwa na mamlaka waliyokuwa wakiipinga. Leo Kanisa linashikilia msimamo huo huo na halitabadilika. Kile tunachokikemea ni utumiaji mbaya wa vyombo vya sheria."

Soma zaidi: Congo kuzinduwa sensa ya watu na vitambulisho vya uraia

Upinzani waunga mkono Kanisa

Kauli ya Askofu Donatien Tshole iliungwa mkono na upinzani uliomkumbusha pia Rais  Tshisekedi kwamba ni wajibu wake  kuhakikisha uchaguzi wa kuaminika na wa uwazi utafanyika katika muda unaoruhusiwa na katiba.

"Maaskofu wanaukosoa mchakato wa uchaguzi ulioanza vibaya, ratiba mbaya ya uchaguzi pamoja na kuundwa wanamgambo wa kisiasa ili kufanya fujo wakati wa uchaguzi. Ni ukweli. Jukumu la Kanisa ni kuwa upande wa ukweli na sio katikati ya msitu ambao Felix anaunda." Alisema Prince Epenge, mmoja wa wasemaji wa muungano wa upinzani, Lamuka.

Viongozi wa upinzani nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Martin Fayulu na Matata Ponyo.

Soma zaidi: Upinzani DRC wamuonya Rais Tshisekedi

Hayo yamejiri huku Tume Huru ya Uchaguzi (CENI) ikifungua ofisi 171 kote nchini Kongo ili  kupokea na kushughulikia maombi  ya wagombea katika uchaguzi wa wabunge wa kitaifa.

Imetayarishwa na Jean Noel Ba-Mweze/DW Kinshasa
 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW