1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kanisa Katoliki Ujerumani lapinga mrengo mkali wa kulia

23 Februari 2024

Maaskofu wa Ujerumani wana wasiwasi juu ya msimamo mkali wa mrengo wa kulia na wamejitenga wazi wazi na chama cha AfD. Hatua isiyo ya kawaida, kwa sababu kawaida hawapendi kutoa maoni kuhusu vyama vya siasa.

Kampeni za uchaguzi wa AfD mbele ya Kanisa Kuu la Freiburg
Wawakilishi wa makanisa nchini Ujerumani wamejitokeza kuchukua msimamo dhidi ya mrengo wa kulia.Picha: Rolf Haid/picture alliance

Maaskofu wa Kikatoliki waliokutana katika mji wa Augsburg wiki hii wamelaani vikali ongezeko la nadharia za utaifa wa kikabila na itikadi kali za mrengo wa kulia katika jamii ya Ujerumani.

"Vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia na vile vinavyokumbatia itikadi hii kwa hivyo haviwezi kuwa mahali pa shughuli za kisiasa kwa Wakristo na pia haviwezi kuchaguliwa," walisema katika taarifa.

Katika nukta hii, maaskofu waligusia kwa uwazi chama cha mrengo wa kulia cha Alternative for Germany (AfD). Walisema imani za chama hicho "hazipatani na sura ya Kikristo ya Mungu na wanadamu."

Kauli hiyo si ya kawaida sana kwa sababu kwa miaka 25 iliyopita, maaskofu wa Kikatoliki wamekuwa wakisitasita kutoa tathmini yoyote ya vyama vya kisiasa.

Mkuu wa Baraza la Maaskofu, Askofu Georg Bätzing, alieleza kwamba maaskofu zaidi ya 60 walijadili kwa muda mrefu juu ya kutoa tamko, lakini walikubaliana kwamba ilikuwa muhimu. Pia amedokeza kuwa tamko hilo limepitishwa kwa kauli moja.

"Baada ya mibubujiko kadhaa ya itikadi kali," taarifa hiyo inasomeka, "AfD sasa imetawaliwa na mtazamo wa utaifa." Inaendelea kubainisha kwamba AfD inazunguka kati ya misimamo mikali ya kweli ya mrengo wa kulia, ambayo shirika la kijasusi la ndani limebaini katika baadhi ya matawi ya kikanda na katika jumuiya ya vijana ya chama hicho, na upopulisti wa mrengo wa kulia.

Taarifa hiyo inalaani hasa chuki dhidi ya wakimbizi, wahamiaji na Waislamu, na "kwa kiwango kinachoongezeka" Wayahudi.

Tamko dhidi ya mrengo wa kulia ilipitishwa kwa kauli moja katika mkutano wa Augsburg.Picha: Annette Zöpf/EPD-Bild/picture alliance

Maaskofu walionyesha kuwa watawawajibisha wafanyakazi wa kanisa na watu wanaojitolea. "Zaidi ya hayo, usambazaji wa kauli mbiu za itikadi kali za mrengo wa kulia - ambazo zinajumuisha ubaguzi wa rangi na chuki dhidi ya Wayahudi - haziendani na huduma ya wakati wote au ya kujitolea katika Kanisa."

Muungano wa kidini dhidi ya mrengo wa kulia

Mapema mwezi wa Desemba, Kanisa la Kiprotestanti nchini Ujerumani pia lilitoa tamko kuhusu AfD, na kutangaza kwamba msimamo wa chama hicho "hauambatani kwa vyovyote na kanuni za imani ya Kikristo." Jumuiya za Wayahudi na Waislamu pia zimetoa maonyo, katika ishara kwamba kuna muungano mpana wa kidini dhidi ya AfD.

Ujerumani imeshuhudia miezi miwili ya maandamano makubwa mitaani dhidi ya matamshi ya chuki na maono ya kisiasa ya mrengo wa kulia wa Ujerumani.

Soma pia: Maandamano dhidi ya itikadi kali za mrengo wa kulia yaenea vijijini

Walianza baada ya ripoti iliyochapishwa Januari 10 na shirika la uandishi wa habari za uchunguzi la Correctiv kuhusu mkutano wa watu mbalimbali wanaofuata mrengo wa kulia na wanasiasa wa mrengo mkali wa kulia, wakiwemo baadhi ya wanachama wa AfD, wakijadili kufukuzwa kwa mamilioni ya watu wenye asili ya uhamiaji wanaoishi Ujerumani.

Maaskofu kadhaa hivi karibuni wameshiriki katika maandamano haya dhidi ya itikadi kali za mrengo wa kulia. Bätzing alishiriki katika maandamano katika jiji lake la maaskofu la Limburg, huku askofu wa Mainz, Peter Kohlgraf, akionya dhidi ya chuki dhidi ya wageni kwenye maandamano katika mji mkuu wa jimbo la Rhineland-Palatinate, Mainz. Huko Augsburg, Askofu Bertram Meier alitangaza upinzani wa kanisa dhidi ya siasa za udhalilishaji na kupinga demokrasia.

Askofu Gerhard Feige wa Magdeburg pengine alikuwa mzungumzaji zaidi, akionya dhidi ya "wahemshaji" na "wabinafsi." Alionya: "Tusikubali uwongo, upotoshaji wa ukweli, na 'sumu ya suluhisho rahisi!'"

Wakristo wa Ujerumani wamekuwa wakizungumza dhidi ya mrengo wa kulia kwa kutumia kauli mbiu 'msalaba wetu hauna ndoano' (ikimaanisha ishara ya swastika ya Manazi)Picha: Bernd Wüstneck/ZB/dpa/picture alliance

Wakatoliki katika eneo la mashariki mwa Ujerumani, ambako chama cha AfD kinatazamiwa kuwa na nguvu kubwa ya kisiasa baada ya uchaguzi wa wabunge katika majimbo matatu baadaye mwaka huu, wamekuwa na sauti kubwa kuliko wenzao wa Magharibi na wamezungumza kwa uwazi kuhusu AfD.

Claudio Kullmann, mkuu wa Ofisi ya Kikatoliki mjini Erfurt na ofisi ya ushirika ya kanisa kwa siasa za serikali kwa miaka sita iliyopita, alikuwa mmoja wa watoa mada katika mkutano wa maaskofu mjini Augsburg. Erfurt iko katika jimbo la mashariki la Thuringia, ambapo AfD kwa sasa inakubalika kwa zaidi ya asilimia 30, ingawa tawi la jimbo la chama hicho limeainishwa kama "lililothibitishwa kuwa na siasa kali za mrengo wa kulia na idara ya upelelezi.

Kullmann alisema kuwepo kwa maadili ya utaifa na mawazo kama ya AfD kunahatarisha mshikamano wa kijamii na "kunaweza hata kuondoa uaminifu miongoni mwa marafiki."

Soma pia: Hofu ya "fashisti" kuongoza serikali ya jimbo Ujerumani

Uamuzi wa Augsburg bila shaka utaongeza msisimko wa Siku ya Kikatoliki ya mwaka huu wa 2024. Kuanzia Mei 29 hadi Juni 2, Wakatoliki watakusanyika Erfurt, wiki 13 pekee kabla ya uchaguzi wa Thuringia - huku Björn Höcke mwenye msimamo mkali wa mrengo wa kulia akiwa mgombea mkuu wa AfD. Kulingana na uamuzi wa mahakama, mwanasiasa huyo mwenye itikadi kali wa AfD anaweza kuitwa fashisti.

Kwa nini chama cha AfD ni maarufu mashariki mwa Ujerumani ?

03:40

This browser does not support the video element.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW