1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kanisa la Kiangalikana laishutumu serikali ya Kenya

19 Novemba 2024

Siku chache baada ya viongozi wa Kanisa Katoliki nchini Kenya, kuikosoa serikali ya Rais William Ruto dhidi ya ufisadi, wenzao wa Kanisa la Kiangalikana pia wameishutumu serikali hiyo kutotekeleza ahadi kwa wananchi.

Kenia | Kirche in Nairobi
Watembea kwa miguu wakipita Kanisa Katoliki la St Peters Clavers katika mtaa wa Uyoma, Nairobi Kenya.Picha: Donwilson Odhiambo/ZUMA Wire/IMAGO

Aidha, kundi la viongozi wa kidini wa Kanisa la Kiangalikana eneo la Nyanza Magharibi ya Kenya wametangaza kufanya maombi ya kitaifa kulaani kile kinachoendelea nchini na pia dhidi ya viongozi wa kisiasa wanaoshiriki ufisadi.

Kupitia ilani kwa vyombo vya habari, uongozi wa Kanisa la Kianglikana nchini Kenya kupitia Askofu Mkuu Jackson Ole Sapit ameikosoa serikali ya Ruto kwa kushindwa kutekeleza ahadi walizozitoa kwa Wakenya huku akiwataka viongozi serikalini kuonyesha unyenyekevu kwa kuyasikiliza malalamiko ya Wakenya yanayofungamana na utozaji ushuru wa juu, kuyumba kwa sekta ya afya kufuatia uhamisho wa mfumo wa NHIF hadi SHA, mfumo mbovu wa malipo katika vyuo vikuu, ongezeko la visa vya utekaji nyara, na mauaji miongoni mwa masuala mengine ya kitaifa.

Miito zaidi ya kanisa dhidi ya serikali ya Kenya

Kufuatia msimamo huu wa Kanisa la Kiangalikana, kundi moja la viongozi wa kanisa hilo pia kutoka eneo la Nyanza Magharibi mwa Kenya wakiongozwa na Askofu wa Dayosisi ya Maseno Magharibi, eneo la Nyanza, John Mark Godia wamesimama na kauli ya wenzao wa Kanisa Katoliki dhidi ya serikali wakiwakosoa wanaoonekana kuwashutumu viongozi wa kanisa dhidi ya msimamo wao kwa serikali.

Rais wa Kenya William Ruto akizungumza baada ya hafla ya kuapishwa kwa Naibu Rais wa Kenya Kithure Kindiki.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Zaidi Askopfu huyo alisema "Mheshimiwa Sholei anastahili kupunguza kujipiga kifua na matamshi dhidi ya watu anaowataja kuwa wanaoipinga serikali, wanastahili kupunguza kasi yao kuwakabili maaskofu wa Kikatoliki na viongozi wa kanisa pindi tunapozungumza dhidi ya ufisadi nchini." Askofu Godia alisema.

Kadhalika, viongozi hao wa kidini wametangaza kufanya maombi ambapo pamoja na mambo mengine wametishia kutoa laana na kuwakemea viongozi wa kisiasa wanaoshiriki ufisadi, wakishikilia kuwa huu sio wakati wa kanisa kuombea miujiza bali kushinikiza uwazi na suluhu kwa chagamoto za kitaifa.

Kauli sawia na hiyo imetolewa na Askofu kanisa la Christ Africa Edwin Ogolla ambaye amehusisha ,mfululizo wa mauaji ya kiholela, utekaji nyara na ukosefu jumla wa usalama nchini na kulegalega kwa asasi za serikali.

Soma zaidi: Naibu mpya wa rais Kenya Kithure Kindiki aapishwa rasmi

Viongozi hao pia wameikosoa hali ya kisiasa nchini iliyobuni ushirikiano wa serikali na upinzani kuchangia kuzima sauti ya kuwatetea wanyonge.

Viongozi hao wa kidini ambao wamesisitiza kuwa, kamwe hawatotishwa na vitisho wameendelea kuishinikiza serikali kuongeza juhudi zinazotumika katika masuala binafsi ya viongozi wa kisiasa mfano nguvu iliyowekwa kumuondoa aliyekuwa Naibu wa Rais Rigathi Gachagua kutatua changamoto zinazowakabili Wakenya.

DW Kenya