1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kanisa la KKKT launga mkono mkataba wa DP World ya Dubai.

21 Agosti 2023

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania, KKKT, limesema linaunga mkoni mkataba wa bandari kati ya serikali ya Tanzania na kampuni ya DW World ya Dubai.

Tansania | Hafen in Dar es Salaam
Picha: Xinhua/picture alliance

lakini kanisa hilo limetoa wito wa kuzingatiwa kwa maoni ya watu wengine yanayotolewa katika majukwaa mbali mbali.

Askofu wa kanisa hilo, Dk. Fredrick Shoo, ameyasema hayo mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyehudhuria maadhimisho ya miaka 60 ya kanisa la KKKT yaliyofanyika Arusha Tanzania ila kiongozi huyo wa nchi amesisitiza kuwa ataendelea na msimamo wa kubakia kimya na kutojibizana na wanaohoji mkataba huo.

Rais Samia Suluhu Hassan wa TanzaniaPicha: Ericky Boniphace/AP/picture alliance

Kwenye ukumbi uliojaa waumini na viongozi wa Kanisa la Kilutheri hapa mjini Arusha, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, alijizuwia kuzungumzia moja kwa moja juu ya ukosoaji dhidi ya mkataba wa bandari ambao umegeuka kuwa ajenda kubwa ya kisiasa, kijamii na kidini hapa nchini, ingawa alitumia jukwaa hilo kusisitiza msimamo wa kulinda usalama, utulivu na umoja wa nchi.

Rais Samia: Nipo tayari kushauriana na viongozi wa dini.

Rais Samia aliyekuwa mgeni rasmi katika maadhimisho hayo amepongeza ushirikiano miongoni mwa taasisi za dini na serikali ya Tanzania na kuahidi kuuendeleza na kuwa tayari kushauriana na viongozi wa dini na madhehebu zote.

Hotuba ya Rais Samia ilitanguliwa na Mkuu wa Kanisa la Kilutheri hapa nchini, Baba Askofu Friedrick Shoo, ambaye aligusia kwa kina juu ya msimamo wa kanisa lake kuelekea mkataba huo, ambao mjadala wake unatajwa kuipasua nchi.

Mtazamo wa kanisa la KKKT kuhusu mktaba wa bandari.

Kauli hiyo ya Askofu Dk. Shoo inakuja wakati ambapo Kanisa Katoliki lenye waumini wengi zaidi nchini Tanzania, kutoa waraka wa kupinga mkataba huo wa bandari, ambao hapo jana Jumapili ulisomwa kwenye makanisa yote.

Ingawa katika hotuba yake, Askofu Dk. Shoo hakuutaja moja kwa moja waraka huo wa Kanisa Katoliki, lakini ameonekana kupingana nao, na kumtaka Rais Samia kuwa mvumilivu na mwenye busara katika kushughulikia maoni ya watu kuhusu mkataba huo wa Bandari.

Soma zaidi:Slaa aachiwa huru kwa dhamana

Kanisa la KKKT lenye waumini wanaofikia milioni 8 na majimbo 27 kote nchini hapa, lilianzishwa mwaka 1963 baada ya muungano wa makanisa saba ya Kilutheri Tanzania.

DW Arusha