Kanisa la Orthodox la Urusi laanza kupata ushawishi Afrika
23 Machi 2026
Kwa miaka mitatu sasa, waumini katika Jamhuri ya Afrika ya Kati wamekuwa wakikusanyika kwenye kwa ajili ya huduma za kiroho za Kanisa la Orthodox la Urusi kwenye parokia ndogo ya Mtakatifu Andre de Bimbo karibu na mji mkuu, Bangui.
Patrick, mwanamme mwenye umri wa miaka 38, ni mmoja wao. Alikuwa mfuasi wa Kanisa Katokili la Kirumi kabla ya kujiunga na Kanisa hili la Orthodox la Urusi, ambalo anasema amejiunga nalo kwa kuwa anayapenda mafundisho yake ya Biblia, na pia jinsi viongozi wa kanisa hilo wanavyozungumza na waumini wao, na vile wanavyowapa muongozo wa kiroho kupitia sala.
Patrick anaongeza na hapa namnukuu: "Tangu kuhamia huku, nahisi mabadiliko chanya yanatokea maishani mwangu. Najihisi niko nyumbani kwenye kanisa langu jipya, imani yangu mpya, na nitaendelea kuiandama njia hii hii." Mwisho wa kumnukuu.
Olive, mwenye umri wa miaka 35, anasema pia anafurahi kuwa muumini mpya wa jamii hii ya kanisa. Naye pia anavutiwa na namna mahubiri yanavyotolewa akisema yanampa mafunzo mema. Akizungumza na DW, amesema na hapa namnukuu: "Sote tunamuabudu Mungu yule yule, na najihisi niko nyumbani kwenye mahubiri yao na vile watu wanavyoalakiana na kanisa hili." Mwisho wa kumnukuu.
Hata kama ibada kuu huwa inafanyika kwa Kirusi, waumini huwa wanaupata ujumbe wake kwa kuwa kanisani hapo huwa na wafasiri wa lugha hiyo kwenda lugha za wenyeji.
Parokia ya Mtakatifu Andre de Bimbo inaongozwa na Baba Askofu Marcel Voyemawa, ambaye mwenyewe alihamia kanisa hilo akitokea Kanisa la Orthodox la Kigiriki.
Kijiografia, makanisa ya Orthodox huwa yanaratibiwa kwa parokia, ambapo bara zima la Afrika linazingatiwa kuwa Parokia ya Alexandria na hivyo kuwa sehemu ya Kanisa la Orthodox la Kigiriki. Voyemawa anaitetea imani ya kanisa lake jipya akitumia kituo cha redio cha kanisa hilo kiitwacho Lengo Songo.
Anasema hapa na namnukuu: "Hapa tuna theolojia halisi ya imani. Kanisa la Orthodox linaundwa na makanisa huru, ambayo kila moja lina mila zake za kienyeji. Kinachowaunganisha kiko juu ya kila kitu, ni lugha ya ibada kwa Mungu." Mwisho wa kumnukuu.
Parokia hii ndogo ya Mtakatifu Andre de Bimbo ni mojawapo tu kati ya nyingi ambazo Kanisa la Orthodox la Urusi limekita mizizi yake. Kwa mujibu wa Kanisa hilo, kuna parokia 350 katika zaidi ya mataifa 30 barani Afrika.
Katika nchi kama Afrika Kusini, Tanzania, Uganda na Kenya, makanisa hayo yanajengwa kwa muundo ule ule wa makanisa ya Mtakatifu Petersburg yakijitafautisha na makanisa yaliyopo hapo tangu zamani.
Kwa wengine, hii ni ishara kuwa Urusi inataka kuonekana uwepo wake, sio tu kupitia mikataba ya ulinzi, jeshi na miradi ya uchimbaji madini, bali kwenye maisha ya watu wa kawaida mitaani.