1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
HistoriaAfrika

Kanku Musa: Tajiri wa dhahabu

Yusra Buwayhid
14 Februari 2021

Mfalme wa Mali, Kanku Musa, anatajwa kuwa mtu tajiri kuwahi kuishi duniani. Aliugeuza Timbuktu kuwa mji mashuhuri Afrika. Alitawala kutoka 1313 hadi 1337.

Kanku Musa: Mfalme tajiri wa dhahabu

02:01

This browser does not support the video element.

Kitu gani muhimu cha kukijua kuhusu Kanku Musa?

Kanku Musa alizaliwa mnamo mwaka 1280 Manden. Na, ingawa kwa wengi anajulikana kama Kankan Musa, lakini ‘Kankan' limepotolewa kutoka jina lake halisi ambalo ni "Kanku”. Hili ni jina la kike ambalo ni la mama yake: Katika baadhi ya makabila makuu wakati huo wanawake walikuwa ndiyo wenye nguvu, kwa hivyo mtoto wa kiume pia alibeba jina la mama yake. Mnamo mwaka 1313, kufuatia kifo cha kaka yake Abu Bakr II, Musa alikuja kuwa kiongozi wa Himaya ya Mali. Wakati wa utawala wake wa muongo mzima, aliusambaza Uislam pamoja na utamaduni wa dini hiyo kote nchini Mali. Na himaya hiyo ikawa yenye mafanikio makubwa kote ulimwenguni.

Asili ya Afrika | Kanku Musa

Kwanini Kaku Musa ni maarufu sana?

Kanku ametokea kwenye familia ya kifalme iitwayo Keita, ambayo ilitawala nchini Mali kwa karne nyingi. Alikuwa ni mfalme tajiri aliyejenga taifa lenye nguvu na mafanikio makubwa wakati wa utawala wake. Kulingana na simulizi za asili, babu yake kwa jina la Abu Bakr I alikuwa ni mdogo wake Sunjata Keita, mwasisi wa Himaya ya Mali. Inatajwa kwamba Musa alitawala wakati wa kilele cha mafanikio ya Himaya ya Mali.

Asili ya Afrika | Kanku Musa

Kanku Musa alikuwa na matazamio gani kwenye Himaya ya Mali?

Anajulikana pia kama Mansa ("Mfalme”) Musa, "Mtawala wa Ghanata” au "Bwana wa Migodi ya Wangara”. Kanku Musa alitawa wakati wa kilele cha harakati za kutafuta maliasili. Anatambuliwa kama mtu tajiri zaidi kuwahi kuishi duniani. Utajiri wake unakadiriwa kuwa ulifika dola bilioni 400, kulingana na baadhi ya vyanzo vya kihistoria. Wakati wa utawala wa Kanku Musa, alianzisha uhusiano wa kibiashara na nchi za mbali. Na dhahabu pamoja na chumvi vilikuwa ndiyo vyanzo vikuu vya utajiri katika ufalme wake.

Kwa kiasi gani Kanku Musa alijifaharisha na utajiri wake?

Mnamo mwaka 1324 Kanku Musa alikwenda Makka kuhiji. Msafara wake ulikuwa na watu 60,000, wafanyakazi 12,000 na watumwa, pamoja na wasaidize wengine waliokuwa wamevalia nguo za hariri na kubeba fimbo za dhahabu huku wakisaidia kulinda farasi na mizigo. Safari hiyo ya kifahari ilimpatia umaarufu mkubwa, hasa Afrika Magharibi na Mashariki ya Kati. Katika kila mji uliopita msafara huo, Musa alionyesha ukarimu mkubwa na kugawa sadaka kutoka katika mali yake.

Kanku Musa: Mfalme tajiri wa dhahabu

This browser does not support the audio element.

Kanku Musa anakumbukwa kwa kipi?

Kutokana na utajiri wake, Kanku Musa alijenga majengo mengi ya kiutawala na kiibada kuanzia mwaka 1325. Miongoni mwao ni misikiti, vyuo vya kufundishia Quran pamoja na makasri katika miji ya Timbuktu na Gao. Msikiti wa Sankoré mjini Timbuktu umebakia hadi hii leo na ni ukumbusho wa utajiri wake. Msikiti huo ulianzisha uhusiano mzuri wa kidini na kitamaduni kati ya Mali na mataifa ya Kiarabu. Baadhi ya wanafunzi wa Mali walikwenda Misri na Morocco kusoma dini ya Kiislam, huku baadhi ya wasomi wa Misri na Morocco pia walifunga safari na kuja kusoma katika chuo cha mafunzo cha msikiti wa Sankoré. Kilikuwa ni kitovu cha Utamaduni wa Kiislam katika eneo la Afrika Magharibi.

Ushauri wa kisayansi kuhusu makala hii umetolewa na wanahistoria Profesa Doulaye Konaté, Lily Mafela, Ph.D., na Profesa Christopher Ogbogbo. Mfululizo wa makala za Asili ya Afrika umefadhiliwa na Taasisi ya Gerda Henkel.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW