Mazungumzo yana nia ya kumaliza mkwamo wa kisiasa
26 Januari 2018Kansela Angela Merkel amesema wanatarajia kwenda mbele katika jitihada zao za kuunda serikali na ndio maana ana matumaini juu ya majadiliano hayo huku akisema anaamini hilo linaweza kufikiwa kwa wakati. Miezi minne baada ya kufanyika uchaguzi mkuu nchini Ujerumani bado hakuna serikali mpya. Iwapo mazungumzo na chama cha Social Democratic yatafanikiwa serikali hiyo mpya inatakiwa kukamilika ifikapo wakati wa Pasaka.
"Siku 14 zilizopita tulikamilisha mazungumzo ya kutathmini uwezekano wa kuunda serikali, ni vizuri kwamba leo tunaweza kuanza mazungumzo hayo, lazima tujadiliane wazi ni mambo gani mema yanafaa kwa Ujerumani ya siku za usoni, tutahakikisha kuwa tunajadiliana haraka ili kupata matokea kwa wakati;"alisema Merkel alipokuwa nje ya makao makuu ya chama cha CDU mjini Berlin.
Kwa upande wake kiongozi wa chama cha Christian Sociol Union CSU Horst Seehofer, amesema chama chake kinaingia katika majadiliano kwa moyo mkunjufu lakini akasema huenda majadiliano hayo yasifanikiwe iwapo kilichoafikiwa kitakataliwa na wanachama wa Social Democrat.
Kiongozi wa SPD Martin Schulz anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wanachama wa chama chake kuingia upya katika serikali ya muungano iliyoiongoza Ujerumani tangu mwaka 2013.
Vyama hivyo vitatu yani vyama ndugu vya kihafidhina Christian Democratic Union CDU na Christian Social Union CSU, pamoja na chama cha SPD wana nia ya kumaliza majadiliano hayo ndani ya wiki mbili ambapo baadaye mpango watakaoafikiana utapelekewa wanachama wa SPD ili kuidhinishwa.
Lakini bado kuna wasiwasi wa Ujerumani kurejea tena katika uchaguzi mpya iwapo majadiliano hayo hayatafua dafu.
Hata hivyo Kansela huyo wa Ujerumani wa muda mrefu alijaribu kuunda serikali na chama cha walinzi wa mazingira die Grüne na waliberali wanaowapendelea bishara chama cha Free Democrats jaribio ambalo lilishindwa mwaka uliopita.
Chama cha kihafidhina cha Kansela Angela Merkel cha Christian Democratic Union CDU, chama cha Bavaria CSU na chama cha Social Democrats wote walifanya vibaya katika uchaguzi uliyofanyika mwezi Septemba mwaka jana hatua ambayo ilikipa chama cha cha siasa kali cha AFD kinachopinga uhamiaji kujipatia umaarufu.
Mwandishi: Amina Abubakar/Reuters/AP
Mhariri: Yusuf Saumu