Kansela Merkel amkaribisha rais Deby wa Chad
12 Oktoba 2016
Katika mkutano na waandisi wa habari mwishoni mwa mazungumzo yao mjini Berlin,kansela Angela Merkel ameahidi serikali yake itaisaidia Chad kukabiliana na kitisho cha kuzidi harakati za wafuasi wa itikadi kali katika eneo hilo na wimbi la wakimbizi wanaokimbia kitisho hicho."Tunaivulia kofia Chad katika juhudi zake za kupambana na ugaidi na juhudi zake za kukabiliana na changamoto zinazolikabili bara la Afrika" amesema kansela Merkel.
Chad inazungukwa na maeneo yanayozongwa na mizozo mfano wa eneo linalopakana na ziwa Chad,Libya na Sudan ameeleza kansela Merkel katika mkutano na waandishi habari. Ameongeza kusema Chad imewapokea wakimbizi laki saba kutoka nchi nyengine za eneo hilo.
Chad ni mfano wa kuigwa barani Afrika
Kansela Merkel amezungumzia pia umuhimu wa kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kukumbusha hadi wakati huu hakuna bado kampuni lolote wala taasisi yoyote ya misaada ya ujenzi mpya inayoendesha shughuli zake katika nchi hiyo. Amesema ameyahimiza makampuni ya Ujerumani hata kabla ya kuondoka kuelekea Afrika yawajibike zaidi barani Afrika. Kansela Merkel amesifu juhudi za serikali ya Chad kuinua elimu kwa wasichana na kurefusha umri wa watoto wa kike kuolewa kuanzia miaka 18 pamoja pia na kuimarisha nafasi ya mwanamke katika jamii:"Huu ni mfano mzuri wa kuigwa barani Afrika" amesema kansela Merkel aliyeahidi.
"Ujerumani itatenga Euro milioni 8.9 za ziada kusaidia kukabiliana na matatizo ya ukosefu wa maji na chakula" .Kwa upande wake Rais Deby amekumbusha tatizo la wahamiaji akisema hawapitii pekee Mali na Niger wanapokuwa njiani kuelekea Ulaya bali wanapitia pia Chad . "Kuna hatari ya kuenea mzozo wa wakimbizi ikiwa Niger tu ndiyo itakayosaidiwa. Muhimu ni kutolewa msaada kwa eneo lote la Sahel. Idriss Deby amezungumzia pia madhara yanayotokana na mashambulio ya kigaidi ya Boko Haram katika eneo linalopakana na ziwa Chad.
Waimla hawawezi kuyapatia ufumbuzi matatizo ya Afrika
Ziara ya Idriss Deby mjini Berlin ni ya kwanza kuwahi kufanywa na rais wa Chad tangu nchi hiyo ya Afrika kati ilipojipatia uhuru mwaka 1960.Wanaharakati wa haki za binaadam wanakosoa ziara hiyo na kusema "ufumbuzi wa mizozo ya Afrika hauwezi kupatikana kupitia watala wa kimabavu."
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri: Iddi Ssessanga