1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Angela Merkel asisitiza maridhiano bungeni

4 Julai 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amelihutubia bunge kwa mara ya kwanza tangu alipokubaliana na waziri wake wa mambo ya ndani Horst Seehofer kuhusu suala la Wahamiaji. Merkel amesisitiza mshikamano.

Deutschland Haushaltsdebatte im Bundestag in Berlin
Picha: Reuters/H. Hanschke

Mikutano ya aina hiyo bungeni mara nyingi hutumiwa na serikali kuhalalisha au kuthibitisha sera zake na kwa upande wa upinzani ndio huwa wakati muafaka wa kurusha maswali ambayo mara nyingine humpa muhusika kigugumizi katika kuyajibu.

Hotuba ya bibi Merkel ilikuwa ni fursa ya kujionyesha kuwa uwezo wake wa kuongoza bado ni imara. Kansela Merkel alitolea mfano makubaliano aliyoyafikia wiki iliyopita katika mkutano wa kilele wa Umoja wa Ulaya nchini Ubelgiji, akisema kuwa waliyaweka sawa maslahi mbalimbali ya Umoja huo juu ya suala la uhamiaji. Kansela Merkel amesema alisisitiza haja ya kuilinda mipaka ya nje ya Ulaya na kuhakikisha ushirikiano na mataifa ya Afrika katika kupambana na uhamiaji haramu.

Lakini mazingira katika bunge la Ujerumani yalikuwa katika hali ya wasiwasi hapo jana Jumanne baada ya kutokuwepo na maelewano juu ya sera ya wahamiaji hali iliyotishia kwa siku kadhaa kuugawa muungano wa kansela Angela Merkel na yumkini kuvunjika kwa serikali.

Kwa sasa kansela Merkel anazungumza na washirika wake katika serikali ya mseto wa chama cha SPD ili kupata ridhaa yao kuhusu mpango wa uhamiaji uliofikiwa na chama chake cha kihafidhina cha CDU na chama ndugu cha Bavaria cha CSU.

Mwenyekiti wa SPD Andrea Nahles Picha: picture-alliance/dpa/B. v. Jutrczenka

Mwenyekiti wa chama cha SPD, Andrea Nahles ameulaumu muelekeo wa waziri wa mambo ya ndani Horst Seehofer na amesema serikali haikuhitaji mipangilio yoyote maalum kwa ajili ya kurekebisha mbinu za serikali ya Ujerumani kwa wanaotafuta hifadhi. Nahles pia alisisitiza kuwa msingi wa sera ya serikali utabakia katika makubaliano ya umoja yaliyosainiwa mwezi Machi na sio mikataba yoyote iliyofikiwa na wahafidhina peke yao.

Wawakilishi wa chama cha SPD watakutana na washirika wenzao wanaounda serikali ya mset hapo kesho Alhamisi kujaribu kufikia makubaliano ya pamoja juu ya sera ya uhamiaji itakayo umaliza mgogoro unaoikabili serikali inayoongozwa na kansela Angela Merkel.

Mwandishi: Zainab Aziz/p.dw.com/p/30mVN

Mhariri: Iddi Ssessanga