1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Markel aelekea Urusi

Mohammed Abdulrahman16 Januari 2006

Ziara yake imekuja siku chache baada ya kuizuru Marekani wiki iliopita.

Bibi Merkel akizungumza jambo na Rais Putin
Bibi Merkel akizungumza jambo na Rais PutinPicha: dpa/AP Combo

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel, anaitembelea Urusi leo, ambako anatarajiwa kufafanua juu ya kuendelezwa ushirikiano ulipo na nchi hiyo, bila ya kuutia dosari urafiki wa karibu uliokuweko kati ya mtangulizi wake Gerhard Schroder na Rais Vladimir Putin.

Bibi Merkel ambaye Ijumaa iliopita alikua na ziara ya kwanza mjini Washington-Marekani na mazungumzo na Rais George W. Bush anatarajiwa kumshinikiza Rais Putin juu ya haja ya kiongozi huyo kusimama kidete upande wa nchi za magharibi, katika mzozo juu ya mpango wa kinuklea wa Iran.

Muhimu zaidi ya yote, atatafuta uungaji mkono kutaka suala la kuanza tena kwa mpango wa utafiti wa kinuklea wa Iran, liwasilishwe mbele ya Baraza la usalama la Umoja wa mataifa- hatua ambayo China na Urusi zimeipinga hapo kabla.

Mjini Washington wiki iliopita, Kansela huyo wa Ujerumani alisema nchi za magharibi hazitoyumbishwa na uamuzi wa Iran wa kuendelea na mpango wake wa kinuklea na kwamba Iran sasa imevuka mpaka.

Kwa mujibu wa mtaalamu mmoja wa uhusiano kati ya Urusi na Ujerumani katika baraza la Ujerumani juu ya uhusiano na nchi za nje, Alexander Rahr huenda Kansela Merkel akaitaka Moscow kuhakikisha nishati yake ya gesi haitumiwi kama silaha ya kisiasa.

Ingawa ni suala la mabishano makubwa, Bibi Merkel hatokua na malalamiko yoyote juu ya ujenzi wa bomba la gesi bahari ya Baltic, ili kuipatia Ujerumani gesi kutoka Urusi. Kwa wakati huu Ujerumani hutegemea asili mia 35 ya gesi ya asili kutoka Urusi.

Wadadisi wanaamini ziara hii fupi ya Bibi Merkel ni jaribio la Kansela ambaye alikulia Ujerumani mashariki ya zamani iliokua ya kikoministi, kuunda uhusiano wa kikazi na Rais Putin, licha ya kwamba haitokua na bashasha iliokuweko wakati wa Kansela aliyemtangulia Gerhard Schroder.

Bw Rahr anasema apende asipende , Bibi Merkel atalazimika kuizingataia mno Urusi, kwa sababu Ujerumani inabakia kuwa kiunganisho mubhimu kati ya Urusi na Ulaya.

Kwa upande mwengine Kansela ana azma ya kuifanya Ujerumani kuwa tena nguvu ya kutegemewa barani Ulaya. Binafsi akizungumza katika mahojiano na jarida la Der Spiegel, Bibi Merkel alisema hafikirii kwamba kuna mengi ya uadilifu ambapo Ujerumani inafanana na Urusi, lakini pamoja na hayo Ujerumani ina masilahi ya kuiona Urusi inaendelea katika njia muwafaka.

Chama chake cha Christian Democratic Union-CDU, kimemtaka Bibi Merkel kuzungumzia bayana juu ya masuala muhimu yanayosababisha kuwepo kwa tafauti ziliopo kati ya Urusi na Ulaya, na hasa uhuru wa vyombo vya habari, jumuiya za kiraia na upinzani wa kisiasa. Kwa mfano Ruprecht Polenz, Mwenyekiti wa kamati ya CDU ya masuala ya nchi za nje katika bunge la Ujerumani –Bundestag, anasema angependelea kuona bibi Merkel akiiambia Urusi kwamba “ Ule mtindo wa zamani wa kufikiri ambao ulisababisha kuundwa maeneo yenye ushawishi wake sasa umepitwa na wakati."

Mengine yanayotarajiwa kuwa huenda yakawa katika ajenda ya mazungumzo ya Merkel na Putin mbali na suala la Iran ni pamoja na Chechnya. Aidha Bibi Merkel atakutana na wanasiasa wa upinzani na wanaharakati, huku vyama vya kisiasa nchini Ujerumani vikimtaka ashinikiza juu ya ukandamizaji wa haki za binaadamu nchini Urusi.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW