1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel amnadi mgombea ukansela Armin Laschet

7 Septemba 2021

Uchunguzi wa karibuni wa maoni unaonesha vyama vya muungano wa Merkel vinashika nafasi ya pili huku chama social Democratic SPD kikitangulia mbele, shukuran kwa umaarufu wa mgombea wake, waziri wa fedha Olaf Scholz.

Angela Merkel und Armin Laschet
Picha: John Macdougall/AFP/Getty Images

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amemsifu mgombea ukansela wa chama chake Armin Laschet kuwa ndiye chaguo bora kurithi nafasi yake, wakati ambapo uchuguzi wa maoni ya wapigakura ukionesha waziri mkuu huyo wa jimbo la North Rhine-Westphalia akifanya vibaya sana kuelekea uchaguzi mkuu wa mwezi huu.

Laschet ambaye anagombea kupitia muungano wa vyama vya kihafidhina vya CDU na CSU, alikuwa anapewa nafasi ya kuwa kansela ajaye kwa muda mrefu, lakini umaarufu wake umeshuka sana kufuatia mkururo wa makosa kwenye kampeni.

Soma pia:Wagombea ukansela Ujerumani wachuana katika mdahalo wa Televisheni

Merkel ambaye anastafu baada ya kuwa madarakani kwa miaka 16, hakushiriki kinyanganyiro cha kuchagua mgombea wa chama chake katika uchaguzi. Lakini wakati umaarufu wa chama hicho cha Christian Democratic Union ukishuka na kufikia kiwango cha chini kabisaa tangu kumalizika kwa vita kuu ya pili ya dunia, chama hicho sasa kinahimiza matukio mengi iwezekanavyo ya pamoja kati ya Merkel na Laschet.

Uchunguzi wa maoni ulioendeshwa na kituo cha televisheni cha NTV na kutangazwa leo Jumanne, umeonesha wahafidhina wakiwa na uungwaji mkono wa asilimia 19 tu, huku chama cha Social Democratic SPD kikiwa mbele kwa asilimia 25 na chama cha Kijani, ambacho mwanzoni kilioenekana kupendelewa na wapigakura, kikiwa na asilimia 17.

''uaminifu na urari ambavyo Ujerumani inahitaji''

Merkel aliwambia waandishi habari kwamba alikuwa anaongoza jimbo kubwa zaidi nchini Ujerumani kwa ufanisi.Picha: Frank Ossenbrink/imago images

Akizungumza katika kikao cha mwisho cha bunge mjini Berlin leo, Merkel amesema uchaguzi huu unahusu mazingatio ya dhahiri ya kiuchumi na kifedha, "ambayo yataamua mustakabali wa nchi hii, idadi ya nafasi za ajira na ustawi wetu wa pamoja."

"Ndiyo maana mabibi na mabwana, njia bora kwa taifa letu ni serikali inayoongozwa na CDU na CSU ikiwa na Armin Laschet kama Kansela, kwa sababu serikali yake itasimamia utulivu, uaminifu na urari ambavyo ndiyo hasa Ujerumani inavihitaji," alisema kansela huyo.

Soma pia: Armin Laschet: Mgombea ukansela wa CDU

Muungano wa CDU na CSU ulishinda asilimia 33 ya kura katika uchaguzi wa 2017 chini ya Merkel, ambaye anasalia kuwa kipenzi cha Wajerumani walio wengi.

Merkel alionekana sambamba na Laschet wakati wa mkutano wa kilele wa kidijitali siku ya Jumatatu, na pia alimsindikiza mwishoni mwa wiki kwenye ziara ya miji miwili ilioathiriwa vibaya na mafuriko mwezi Julai.

Katika jimbo la North Rhine-Westpahalia, ambako Laschet ndiye waziri mkuu, Merkel aliwambia waandishi habari kwamba alikuwa anaongoza jimbo kubwa zaidi nchini Ujerumani kwa ufanisi.

Soma pia:Maoni: Manifesto ya CDU/CSU haina majibu yanayotosheleza 

CDU/CSU kuhamia upinzani?

Mporomoko wa Lashet ulianzia kwenye namna alivyoshughulikia mafuriko katika jimbo lake, baada ya kuonekana kwenye kamera akifanya utani na maafisa wa serikali wakati wa kutoa heshima kwa wahanga wa mafuriko hayo.

Ikiwa majaaliwa ya muungano wa CDU na CSU hayataboreka haraka, huenda kurejea kwao madarakani ikawa ndoto, na kuupisha muungano unaoongozwa na SPD -- wenye uwezekano wa kujumlisha chama cha Kijani na ama chama cha kiliberali cha FDP au chama cha mrengo wa kushoto cha Die Linke.

Chanzo: Mashirika

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW