1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Merkel atetea makubaliano na Iran bungeni

Sekione Kitojo
16 Mei 2018

Angela Merkel ametetea makubaliano ya kinyuklia na Iran kufuatia kukataliwa na Marekani, na kwamba  mkataba huo ni njia bora ya kupambana na shaka juu ya kujihusisha kwa Iran nchini Syria na mpango wake wa makombora.

Deutschland Bundestag Angela Merkel
Picha: Reuters/H. Hanschke

Katika hotuba yake iliyogusia  mambo  mbali  mbali  katika  bunge  la Ujerumani  Bundestag , kansela  Merkel amezungumzia  masuala kadhaa  kuanzia  mageuzi  ya  msingi  kabisa  hadi ulinzi  na  hatua za  kidigitali,bila hata hivyo kuelezea undani mkakati wa mipango hiyo.

Kansela wa Ujerumani Angela MerkelPicha: Reuters/H. Hanschke

Mtazamo wenye  ncha  nyingi, ikiwa  ni  pamoja  na  kuielekea  Iran , ni  njia  pekee, amesema  Merkel, ambaye pamoja  na  mataifa mengine  ya  Ulaya yanajaribu  kuyanusuru  makubaliano  hayo  ya kinyuklia bila  ya  Marekani.

Merkel  ameyaeleza  makubaliano  hayo  kuwa  nsio kamilifu, lakini akaongeza  kwamba  maafisa wa  kimataifa  wanaohusika  na masuala  ya  kinyuklia  wamesema  Iran  inatekeleza  majukumu yake.

"Hii  haina  maana  kwamba  tunafurahia  kila  kitu  ambacho  Iran inafanya , tunapaswa  kuzungumzia  juu  ya kujihusisha kwa  Iran nchini  Syria , mpango  wake  wa  makombora, na masuala  mengine, lakini  swali iwapo  unaweza  kufanikiwa zaidi  ikiwa utasitisha makubaliano  ama  iwapo unakaa  nje  ya  makubaliano  hayo," Merkel  amewaambia  wabunge leo.

"tunasema  unaweza  kuzungumza  vizuri  zaidi  iwapo  utabakia katika  makubaliano," aliongeza Merkel.

Waziri wa fedha wa Ujerumani Olaf ScholzPicha: picture-alliance/dpa/B. v. Jutrczenka

Uhusiano  kati ya Ulaya  na  Marekani

Wiki  iliyopita, rais  wa  Marekani  Donald Trump  alijitoa  katika makubaliano  ya  mwaka  2015  kati  ya  Iran  na  mataifa  sita yenye  nguvu  duniani  ambayo  yaliondoa  vikwazo vya  kiuchumi vingi  vya  kimataifa  ili Iran iweze  kusitisha  mpango wake  wa kinyuklia, ukiwa  chini  ya  uangalizi  wa  shirika  la  Umoja  wa mataifa  linaloshughulikia  nishati  ya atomiki.

Katika  hotuba  yake Merkel  amedokeza kwamba licha  ya  kuwapo na  matatizo  hivi  sasa, uhusiano  wa  mataifa  ya  Ulaya  na Marekani  utabakia  kuwa  muhimu. Lakini  pia  alitoa  tahadhari.

"Lakini  uhusiano  huu  wa  mataifa  yanayopakana  na  bahari  ya Atlantic  pia  ni  lazima  uwe  na  uwezo  wa  kuhimili  tofauti  ya mawazo, hususan  kama  tunavyoona  siku  hizi  kwa  Marekani kujitoa  kutoka  katika  makubaliano  ya  kinyuklia  na Iran."

Merkel  pia  alitoa  wito wa  kuimarishwa  kwa  kanda  ya  sarafu  ya euro  na  kuweka  uzito  katika  pendekezo  kutoka  kwa  waziri  wake wa  fedha  kutoka  chama  cha  Social democratic SPD, Olaf Scholz kuubadilisha mfuko wa Ulaya  wa  mfumo wa kuleta  uthabiti  ESM, na  kuwa  chombo  kitakachotumika  kukamilisha  kufungwa  kwa mabenki yanayofanya  vibaya.

Spika wa bunge la Ujerumani Wolfgang SchaublePicha: picture-alliance/dpa/G. Fischer

Merkel  na  Scholz wanatofautiana  na   rais  wa  Ufaransa Emmanuel Macron  kuhusiana  na  mawazo  yake  ya msimamo mkali ya  kuweka bajeti  maalumu ya  mataifa  ya  kanda  ya  sarafu ya  euro, na  kumteua  waziri wa  fedha  na  kubadili fuko  hilo  la kuleta  uthabiti  kuwa shirika  la  fedha  la  Ulaya.

Katika  mjadala  bungeni kiongozi  wa  wabunge  wa  chama  cha siasa kali  za  mrengo  wa  kulia cha  Alternative  for  Germany AfD, Alice Weidel , alikaripiwa na  spika  wa  bunge  la  Ujerumani Wolfgang Schaueble  kwa  kuwabagua  wanawake wanaovaa hijabu katika  hotuba  yake.

Mwandishi: Sekione  Kitojo rtre

Mhariri:Gakuba, Daniel

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW