Kansela Merkel atoa mwito wa kujizatiti katika kupambana na umaskini duniani.
20 Septemba 2010Wajumbe kwenye mkutano wa kilele wa siku tatu kwenye Umoja wa Mataifa leo wanaanza kutathmini hatua iliyofikiwa katika juhudi za kupambana na umasikini zilizoanzishwa mwanzoni mwa karne hii.
Miaka 10 iliyopita jumuiya ya kimataifa ilijipa wajibu wa kuyatekeleza malengo ya milenia, ikiwa pamoja na kupunguza kiwango cha umasikini kwa nusu hadi hapo utakapofika mwaka wa 2015.
Viongozi wa nchi na wakuu wa serikali zaidi ya mia moja wanahudhuria mkutano huo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York.
Kabla ya mkutano kuanza, Kansela Angela Merkel wa Ujerumani alitoa mwito wa kujizatiti zaidi katika juhudi za kupambana na umaskini duniani.
Bibi Merkel anahudhuria mkutano huo pamoja na waziri wa maendeleo, wa Ujerumani, Dirk Niebel
Malengo mengine ya milenia ni kupunguza vifo vya watoto kwa theluthi mbili na kutoa fursa zaidi za elimu.Lakini asasi zisizo za kiserikali zimelalamika kwamba nchi tajiri hazitoi mchango zaidi ili kusaidia katika kuleta maendeleo duniani.
Akizungumzia juu ya hatua iliyofikiwa hadi sasa waziri wa mandeleo wa Ujerumani Dirk Niebel amesema ingawa mafanikio ya kutia moyo yamepatikana, bado vifo vya watoto na vya akina mama vimo katika viwango vya juu visivyoweza kuvumilika.