Kansela Merkel atunukiwa tuzo ya Fulbright
29 Januari 2019Sherehe za kutunikwa tuzo ya shirika lenye makao yake mjini Washington la Fulbright zimefanyika kwa mara ya kwanza nje ya Marekani. Miongoni mwa waliohudhuria sherehe hizo ni pamoja na balozi wa Marekani mjini Berlin , mkosoaji mkubwa wa kansela, Grenell. Shirika hilo limesifu uongozi wake unaostahiki kuigwa, na juhudi zake za kupigania hali ya kuelewana, ushiriikiano wa kimataifa na amani."
Katika hotuba yake, kansela Merkel ametilia mkazo umuhimu wa ushirikiano katika kupambana na kuongezeka hisia za uzalendo na kujipendelea, akiutaja mchango wa Marekani baada ya vita vikuu vya pili vya dunia katika kusaidia kurejesha uhuru na demokrasia nchini Ujerumani na Ulaya magharibi.
Jukumu la kulinda uhuru na amani
"Tunabidi tuwajibike kuhakikisha amani inaendelea kuwepo.Tunastahiki kushukuru kwamba katika nchi zetu bado tunajivunia uhuru na amani. Lakini tusipakate mikono tunabidi tuwajibike zaidi na kuwa macho kuangalia yanayotokea katika jamii ndani na nje ya nchi zetu."Amesema kansela Merkel
Bila ya kuutaja kwa jina usemi wa rais wa Marekani Donald Trump- Amerika Kwanza au mvutano kuhusiana na sera zake za kibiashara na masuala mengine kadhaa, kansela Merkel amekosoa hisia za kujipendelea na kusema,"Uzalendo kwangu mie unamaanisha kufikiria masilahi ya kibinafsi pamoja na yale ya wengine. Na ndio maana sitochoka kila mara kutilia mkazo umuhimu wa kuimarishwa maadili na mwongozo wa dunia unaotilia maanani ushirikianao wa pande tofauti.
Merkel aingia katika madaftari ya historia
Kansela Angela Merkel ameingia katika madaftari ya historia kuwa miongoni mwa
viongozi mashuhuri waliotunukiwa tuzo hiyo, wakiwemo Jimmy Carter wa Marekani, Vaclav Havel wa jamhuri ya Cheki na Nelson Mandela wa Afrika Kusini.
Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/dpa
Mhariri: Iddi Ssessanga