Kansela Merkel azuru Brazil
20 Agosti 2015Kansela Angela Merkel wa Ujerumani,waziri wa mambo ya nje Frank - Walter Steinmeier na wanasiasa wengine waandamizi wa Ujerumani wamewasili katika mji mkuu wa Brazil Brasilia hapo jana na ujumbe huo uliondoka nchini Ujerumani kwa ajili ya ziara hiyo mara tu baada bunge la Ujerumani kuidhinisha mpango mpya wa mkopo wa kuinusuru Ugiriki isifilisike na madeni.
Katika ziara hii fupi Kansela Merkel amekutana na Rais Dilma Roussef wa Brazil na wawakilishi wa kibiashara kabla ya kurudi nyumbani Alhamisi.
Serikali za nchi hizo zimesema mazungumzo yao yamejikita kwenye ushusiano wa tekenolojia, sayansi,maendeleo biashara,masuala ya fedha na elimu halikadhalika uhifadhi wa mazingira.
Suala la Mercusor
Merkel akizungumza na waandishi wa habari Alhamisi kuhusu mkutano wake wa Jumatano na Rais Dilma Roussef wa Brazili amesema suala la mazungumzo ya bishara huru ya Mercosur Umoja wa Forodha unaozijumuisha Brazil,Argentina,Paraguay na Uruguay pia limo katika mjadala.
Amekaririwa akisema "Kuna jambo moja ambalo linanitia moyo na linaweza kutilia nguvu ufufuaji wa ushirikiano wa kiuchumi : ni kuwa tayari kwa Brazil kuharakisha mazungumzo hayo juu ya makaubaliano ya biashara huru baina ya Umoja wa Ulaya na Mercosur.Brazil ina matumaini makubwa kadri suala hilo linavyohusika. Suala hili lilikuwa na dhima kubwa katika mzungumzo ya hapo jana na leo hii pia itakuwa hivyo hivyo."
Katika taarifa iliyotolewa kwa njia ya baruwa pepe serikali ya Brazil imesema inataraji ziara hiyo ya Merkel itasaidia Brazil kuimarisha uhusiano wake wa kiuchumi na Ujerumani na Umoja wa Ulaya pamoja na kufunguwa masoko zaidi katika kanda hiyo ya Amerika Kusini.
Uhusiano wa enzi
Ujerumani na Brazil zina uhusiano uliodumu kwa karne nyingi.Hapo Jumatano waziri wa mambo ya nje wa Ujerumani Frank- Walter Steinmeier wakati akijibu suali katika mahojiano na gazeti la Brazil la "Folha de S.Paulo " kuhusu jinsi Ujerumani inavyoiangalia hali tete ya kisiasa iliopo hivi sasa nchini Brazil amesema wahamiaji wa kwanza wa Ujerumani wamewasili Brazil kama miaka 200 iliopita na kwamba kampuni za Ujerumani zimeanza kuwepo nchini humo miaka 150 iiliopita kwa hiyo Ujerumani inachukuwa mtizamo wa muda mrefu wakati linapokuja suala la uhusiano wa nchi hizo mbili.
Ameongeza kusema kwamba Brazil ni na itaendelea kubakia kuwa mshirika wao muhimu kabisa Amerika Kusini bila ya kujali changamoto ziliopo hivi sasa katika siasa za ndani nchini humo.
Mzungumzo ya kiserikali kati ya nchi hizo mbili yanatarajiwa kutowa msukumo katika uhusiano wa nchi hizo mbili. Mikataba 15 iliosainiwa na azimio la pamoja kuhusu mabadliko ya tabia nchi inakusudia kuimarisha ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.Brazil itakuwa miongoni mwa nchi tisa ambazo Ujerumani itakuwa na mawasliano nayo ya kila leo katika ngazi ya mawaziri.
Mwandishi : Mohamed Dahman /DW/AP
Mhariri : Iddi Ssessanga