Kansela Merkel ziarani nchini India
30 Oktoba 2007“Tunataka kupanua na kuimarisha ushirikiano wetu wa kimkakati, na katika kila sekta.” Amesema hayo kansela Angela Merkel ,mjini New- Delhi leo,mwanzoni mwa ziara yake ya siku nne nchini India.
Mbali na sekta za kiuchumi ,kansela Angela Merkel amezitaja pia sekta za sayansi na hifadhi ya hali hewa kua ni miongoni mwa sekta muhimu za ushirikiano kati ya Ujerumani na India.
Kansela Angela Merkel anapigania vizuwizi vya kibiashara na urasimu viondolewe na kuyasihi makampuni ya India yawekeze nchini Ujerumani.
Ametetea pia haja ya kuimarishwa ushirikiano kati ya jumuia ya mataifa manane tajiri kiviwanda G8 pamoja na India ,na mataifa mengineyo pia yanayoinukia.
Kansela Angela Merkel ameendelea kusema: „Tunapendelea kubadilishana fikra na maarifa pamoja na India pamoja pia na maasuala ya utafiti.Makubaliano kadhaa yatatiwa saini,na yatadhihirisha wazi wazi India ni mshirika wetu katika maendeleo ya kisayansi.“
Kansela Angela Merkel aliyewasili New-Delhi jana usiku,na kukaribishwa kwa hishma za kijeshi na waziri mkuu Manmohan Singh hii leo,amefuatana na ujumbe wa watu 140 wakiwemo wakuu wa makampuni kadhaa na wawakilishi wa mashirika ya kisayansi na misaada ya maendeleo.
„Hii pia inaonyesha kwamba ushirikiano kati ya Ujerumani na India si wa „ujia mwembamba“,ni ushirikiano mpanaq na ambao tunataka kuzidi kuuimarisha.“Amesisitiza kansela Angela Merkel.
Katika sekta ya ushirikiano wa kiuchumi kansela anaamini bado kuna nafasi ya kuuzidisha uhusiano huo,ikilinagnishwa na uhusiano pamoja China.Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita,ushirikiano wa kiuchumi kati ya Ujerumani na india ulifikia yuro bilioni kumi nukta tano.Biashara ya öpamoja kati ya Ujerumani na China katika kipindi hicho hicho cha mwaka mmoja uliopita ni mara sabaa zaidi.
Kwa upande wa shughuli za utafiti kansela Angela Merkel anapendelea ushirikiano uimarishwe katika sekta za afya,bioteknolojia,ufundi wa anga za juu na kuhifadhiwa hali ya hewa.
Kansela Angela Merkel anaitembelea India akiwa pia mwenyekiti wa jumuia ya mataifa manane tajiri kiviwanda.Ametetea haja ya kuendelezwa mazungumzo pamoja na mataifa yanayoinukia ambayo mbali na India,ni China,Brazil,Mexico na Afrika kusini.
Hapo awali kansela Angela Merkel na mwenyeji wake,waziri mkuu Manmohan Singh walitia njiani treni ya ufundi wa hali ya juu kwa jina Science Express,inayotazamiwa kuizunguka miji mbali mbali ya India hadi ifikapo mwisho wa mwezi June mwakani.
Baaadae hii leo kansela Angela Merkel atakutana tena na waziri mkuu Manmohan Singht kwa mazungumzo ya kina.Mikataba kadhaa inatazamiwa kutiwa saini kabla ya kansela Angela Merkel kuondoka New-Delhi na kwenda Mumbai hapo kesho.-