Kansela Merkel:Tusiitegemee Marekani katika NATO
13 Januari 2017Umoja huo unakabiliwa na changamoto zinazozidi kuongezeka katika mipaka yake na maeneo jirani ikiwa ni pamoja na uhamiaji, ongezeko la vitisho vya ugaidi, vita nchini Syria, vurugu mashariki mwa Ukraine na umaskini na njaa barani Afrika.
Japo Kansela Merkel hamkutaja Rais mteule Donald Trump kwa jina wakati akieleza changamoto hizo, ilikuwa bayana alikuwa akiyalenga matamshi aliyoyatoa Trump wakati wa kampeini zake kuwa atafikiria upya mchango wa Marekani katika Jumuiya ya NATO kabla ya kutoa msaada wowote.Trump pia aliutaja ushirika huo wa kijeshi wa mataifa ya magharibi kama uliopitwa na wakati.
"Dunia inayokabiliwa na misukosuko,migogoro ya mara kwa mara,mashambulizi ya mitandaoni, hizi ni baadhi ya changomoto zinazotukabili sisi sote. Kwa hivyo ni muhimu kuchukua hatua kwa pamoja.Na ni wazi,na Ujerumani inafahamu hilo,kuwa tunahitaji kutumia fedha zaidi ili bara la Ulaya litimize wajibu wake wa kimataifa sio tu ndani ya NATO bali pia ndani ya Umoja wa Ulaya” alisema Merkel
Mwezi Novemba mwaka uliopita Kansela Merkel alisema Ujerumani lazima iongeze kiwango cha fedha inachotumia katika ulinzi ili kufikia malengo ya jumuiya ya NATO ya asilimia 2 ya pato la taifa, lakini akapuuzilia mbali matarajio kuwa malengo hayo yatatimizwa katika siku za hivi karibuni.
Umoja wa Ulaya ambao umekuwa ukiitegemea Marekani kuuhakikisha usalama wake katika kipindi cha miongo saba,ulikubali kuchukua hatua kuelekea kuimarisha ushirikiano wao wa usalama na ulinzi katika mkutano wa kilele uliofanyika mwezi Disemba. Merkel ambae pia amekosolewa hapa Ujerumani kutokana na sera yake ya milango wazi kwa wakimbizi, pia aliutaka umoja wa ulaya kuharakisha kazi yake katika sajili ya kuingia na kutoka ili kutoa ulinzi unaohitajika mipakani. Kuhusu Uingereza kujiondoa katika Umoja wa Ulaya Kansela Merkel aliwataka wanachama 27 wa Umoja huo waliosalia kuzungumza kwa sauti moja."Kuhusu Brexit, ambayo sisi pia tulizungumzia, ni muhimu kutoruhusu kugawanywa .Lazima tukae meza ya mazungumzo kwa pamoja kama wanachama 27. Lakini kwanza lazima tusubiri majibu kutoka kwa Uingereza inavyotaka kutekeleza Brexit"
Waingereza walipiga kura mwezi Juni mwaka jana kuondoka EU lakini wanachama wa Umoja huo wamekataa kushiriki mazungumzo yoyote kuhusu uhusino wao wa baadae na Uingereza hadi kutekelezwa kipengee cha 50 cha kujiondoa katika Umoja huo.
Mwandishi:Jane Nyingi/AFP/RTRE
Mhariri:Iddi Ssessanga